1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu ahitaji muda zaidi kuunda serikali Israel

1 Machi 2013

Hali ya kukwama mazungumzo pamoja na vyama vinavyotegemewa kuunda serikali ya muungano nchini Israel imemfanya waziri mkuu Benjamin Netanyahu aombe muda zaidi ili kuepukana na kishindo cha kuitishwa tena uchaguzi .

https://p.dw.com/p/17ooh
Rais Peres na waziri mkuu Benjamin NetanjahuPicha: picture alliance / dpa

Duru za kuaminika zinasema waziri mkuu Benjamin Netanyahu atakutana na rais Shimon Peres kesho usiku kumuomba ampatie wiki mbili zaidi baada ya chama chake cha mrengo wa kulia-Likud,kilichopata ushindi mdogo tu katika uchaguzi wa January 22 iliyopita,kumaliza wiki zote nne za mazungumzo bila ya kufanikiwa kuunda serikali ya muungano.

Hata hivyo pindi Benjamin Netanyahu akishindwa kupata washirika wa kutosha kudhibiti wingi wa viti bungeni hadi ifikapo March 16 na kuendelea na wadhifa wa waziri mkuu kwa mara ya tatu,basi rais Shimon Peres anaweza kumkabidhi kiongozi wa chama hasimu jukumu la kuunda serikali.Na ikiwa juhudi zote zitashindwa basi waisrael watalazimika kurejea tena vituoni.

Rais Barack Obama amepanga kuitembelea Israel mwishoni mwa mwezi huu wa Marchi kuzungumzia utaratibu uliokwama wa mazungumzo ya amani pamoja na wapalastina na pia changamoto nyengine zinazolikumba eneo hilo,ikiwa ni pamoja na suala la Iran na mzozo wa Syria.Lakini huenda akaifutilia mbali ziara hiyo ikiwa Netanyahu atashindwa kuunda serikali nchini Israel.

Chama cha Likud cha Benjamin Netanyahu pamoja na kile cha siasa kali za kizalendo cha Israel Beitenu vilijipatia viti 31 katika bunge la Israel-Knesset lenye viti 120.Netanyahu anahitaji angalao wingi wa viti 61 kuweza kuunda serikali ikimaanisha muungano wa vyama vingi ambavyo kila kimoja kina madai na masharti ya aina yake.

Nafuu kwa wayahudi wa nadharia kali

Israel - Orthodoxe Juden protestieren gegen Wehrpflicht
Wayahudi wa nadharia za Orthodox washiriki katika ibada kulalamika dhidi ya kulazimishwa kulitumikia jeshiPicha: picture-alliance/dpa

Benjamin Netanyahu amekabiliwa na upinzani wa vyama vilivyomaliza nafasi ya pili na ya nne Yesh Atid na Bayit Yehudi wanaoshikilia serikali iache kuwaruhusu wayahudi wa nadharia kali wasilitumikie jeshi na iache pia kuwapatia ruzuku kadhaa za kijamii.

Chama cha tatu kikubwa nchini Israel,chama cha Labour kimeondowa uwezekano wa kujiunga na serikali itakayoongozwa na Benjamin Netanyahu.

Utafiti wa maoni ya umma unaashiria pindi uchaguzi mpya ukiitishwa basi vyama vya Yesh Atid na Bayit Yehudi,vinavyodhibiti-cha kwanza viti 19 na cha pili viti 12,vitanyakua viti vingi zaidi kumpita Netanyahu na vyama vyake vya Likud na Israel Beitenu.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/AP

Mhariri:Yusuf Saumu