1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu amaliza ziara yake Marekani

6 Machi 2012

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu leo anahitimisha ziara yake nchini Marekani huku akionya kuwa Israel haitaendelea kukaa kimya huku Iran inaendelea kutekeleza mpango mpango wake sila za nyuklia.

https://p.dw.com/p/14FhT
Rais Barack Obama na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu
Rais Barack Obama na Waziri Mkuu Benjamin NetanyahuPicha: dapd

Baada ya mazungumzo yaliyofuatiliwa kwa karibu sana kati yake na Rais Barack Obama wa Marekani, Netanyahu alisema yeye kama Waziri Mkuu wa Israel, kamwe hatokubali kuona raia wake wanaishi katika hali ya khofu na kuongeza kuwa, Wakati Israel ikisubiri njia za amani zitumike, Iran imeendelea kusonga mbele na mpango wake wa kutengeneza silaha za nyuklia.

Lakini Rais Obama alisema siku ya Jumatatu kuwa, Marekani na Israel zinakubaliana juu ya matumizi ya diplomasia kama njia bora zaidi ya kumaliza mgogoro wa Iran wa nyuklia, ingawa Waziri Mkuu Netanyahu hakuonesha kukubaliana na msimamo huu waziwazi

Rais Barack Obama katika mazungumzo na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu katika Ikulu ya White House siku ya Jumatatu
Rais Barack Obama katika mazungumzo na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: dapd

"Bado tunaamini kwamba dirisha linalowezesha kumaliza mgogoro huu kwa njia za kidiplomasia bado liko wazi. Lakini mwisho wa siku, utawala nchini Irani laazima ufanye uamuzi kuelekea katika njia hiyo. Uamuzi huu bado hawajaufanya," alisema Rais Obama.

Netanyahu Aungwa mkono na wabunge wote

Ingawa Waziri wa mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton, amekuwa akikosoa uamuzi wa Isarael kuendelea kujenga makazi ya walowezi katika ukanda wa Gaza chini ya utawala wa Netanyahu, lakini Waziri Mkuu huyo bado anapata kuungwa mkono na wabunge wa pande zote nchini Marakani.

Netanyahu alisema nchi yake laazima itafanya kila njia kuhakikisha inalinda usalama wake pamoja na wa raia wake. "Israel laazima iwe na uwezo kila wakati kujilinda yenyewe dhidi ya vitisho vyovyote na linapokuja suala la usalama, Israel ina kila haki ya kufanya maamuzi inayoona yanastahili."

Katika mazungumzo yao ya faragha, Rais Obama alisema hataki kuingia vitani na Irani wakati huu, lakini akaongeza kuwa, kama hakutakuwa na njia mbadala ya kuilaazimisha Iran kusitisha mpango wake, basi atalaazimika kufanya hivyo.

Rais wa Israel, Shimon Perez, ambaye alikutana na Rais Obama siku ya Jumapili, alisema alitoka na hisia kwamba Rais Obama sasa alikuwa na nia ya dhati ya kuilaazimisha Iran kuachana na mpango wake wa nyuklia.

Ingawa Israel inasema bado haijaamua kuanza mashambulizi, dalili zinaonesha utayari wake wa kufanya hivyo katika miezi kadhaa ijayo.

Kituo cha kurutubisha Uranium cha Nantanz, nchini Iran
Kituo cha kurutubisha Uranium cha Nantanz, nchini IranPicha: AP

Lakini akosolewa nyumbani

Mbunge wa Bunge la Israel na mwenyekiti w kamati ya Bunge y a mambo ya nje na usalama, Shaul Mofaz, aliikosoa taarifa ya Waziri Mkuu wake kuwa Iran ni tishio kwa Israel, na kuongeza kuwa Iran haiitishii Israel pekee, bali inatishia dunia nzima na hivyo inatakiwa kushugulikiwa na dunia nzima na Israel peke yake.

Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la nguvu za atomiki, Yukiya Amano alisema siku ya jumatatu kuwa shirika lake lina wasiwasi Irani ilikuwa inaficha kazi za siri za atomiki baada ya kushindwa kupata ushirikiano kutoka kwa maafisa wa Iran hivi karibuni.

Wakati huo huo, Mgombea anayeongoza katika kura za maoni kuptia chama cha Republican, Mitt Romney, amekejeli jitihada za Rais Obama juu ya kusimamisha mpango wa Iran wa Nyuklia na kusema kuwa yeye akichaguliwa kuwa Rais wa marekani mwezi November mwaka huu, sera zake madhubuti zitamuezesha kuisimamisha Iran, ingawa wachambuzi wanasema sera zake juu ya suala hili hazitofautiani na za Obama.


Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga\APE\
Mhariri:Mohamed Abdul Rahman.