1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu amwalika Rais Abbas Jerusalem

1 Julai 2010

Waziri Mkuu wa Israel Benjamini Netanyahu amesisitiza wito wake wa kuwa na mazungumzo ya ana kwa ana na wapalestina na kuahidi kuzuru Ramallah iwapo lakini Rais Mahamoud Abbas atakwenda Jerusalem

https://p.dw.com/p/O7Vn
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: AP

Wito huo ameutoa kabla ya kuelekea Washington wiki ijayo kwa mazungumzo na Rais Barack Obama, katika juhudi za kufufuliwa kwa mazungumzo ya amani ya mashariki ya kati.

Akizungumza na waandishi wa habari, mara baada ya mazungumzo yake na mjumbe maalum wa Marekani katika mzozo wa mashariki ya kati George Mitchell,Waziri Mkuu huyo wa Israel amesema anamualika Rais Abbas kwenda Jerusalem, na kwamba naye anajianda kwenda Ramallah.

Mji wa Jerusalem ambao Israel iliutangaza kuwa mji wake mkuu, unapakana na Ramallah ambako ndiko makao makuu ya utawala wa Rais Abbas.Tokea mwezi Mei mwaka huu mjumbe huyo wa Marekani amekuwa akisimamia mazungumzo kati ya viongozi hao wawili, mazungumzo yasiyo ya ana kwa ana.

Wapalestina walisitisha mazungumzo ya amani ya kwa ana kwa ana na Israel, mwaka 2008 baada ya Israel kufanya uvamizi katika Ukanda wa Gaza na kusababisha mauaji ya wapalestina kadhaa.

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amesema anategemea mazungumzo yake wiki ijayo na Rais Barack Obama yataangazia jinsi ya kuanza moja kwa moja mazungumzo ya ana kwa ana na wapalestina.

Naye Waziri wa Ulinzi wa Israel Ehud Barak amesema anatarajia kukutana na Waziri Mkuu wa mamlaka ya wapalestina Salam Fayyad mnamo siku chache zijazo.Ofisi ya Bwana Fayyad imethibitisha kuwepo kwa mkutano huo.

George Mitchell / Nahost / Israel / Palästinenser / USA
Mjumbe maalum wa Marekani katika mashariki ya kati George MitchellPicha: AP

Mapema mjumbe maalum wa Marekani katika mzozo wa eneo hilo,George Mitchell alikwenda Ukanda wa Gaza kwenda kujionea hali ilivyo baada ya Israel kulainisha vizuizi na kuruhusu kuingia kwa misaada ya kiutu.Marekani imepongeza hatua hiyo ya Israel ambapo msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje Philip Crowley amesema hivi sasa kuna malori kati ya 130 na 140 yakiwa na bidhaa yanajianda kuingia Gaza.

Mbinyo wa kimataifa baada ya uvamizi wa meli zilizokuwa na misaada ya kiutu kwa wapalestina wa Gaza mwezi mmoja uliyopita, umeifanya Israel kulegeza vizuizi hiyo.Katika uvamizi huo wanaharakati wanane wa kituruki waliuawa.

Wakati hayo yakiendelea, ndege za kijeshi za Israel zimeshambulia maeneo matatu huko huko Gaza lakini hakuna mtu aliyejeruhiwa.Msemaji wa jeshi la Israel amesema shambulio hilo ni kujibu shambulio la roketi kutokea Gaza ambalo liliharibu kidogo kiwanda kimoja kusini mwa Israel.

Katika hatua nyingine, inaarifiwa kuwa Waziri wa Biashara wa Israel Benjamin Ben Eliezer amekutana kwa siri na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Ahmet Davutoglu, ikiwa ni katika jitahada za kutaka kurejesha uhusiano kati ya nchi hizo mbili.Uhusiano huo umevurugika kutokana na kuawa kwa wanaharakati wa kituruki katika meli ya misaada iliyokuwa ikielekea Gaza.

Kituo kimoja cha televisheni nchini Israel kimesema mawaziri hao walikutana siku chache zilizopita katika eneo moja la siri barani Ulaya.Kituo hicho kimesema, mazungumzo hayo yalikuwa ya siri kiasi kwamba hata wizara ya nje ya Israel haikuhusishwa.

Kutokana na hali hiyo ofisi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel Avigdor Lieberman imeshutumu mazungumzo hayo na kusema ni dharau kwa wizara ya nje.Hata hivyo imeelezwa kuwa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu aliridhia kufanyika kwa mazungumzo hayo ya siri na Uturuki.

Mwandishi:Aboubakary Liongo/AFP/DPA

Mhariri:Sekione Kitojo