1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu asifu hukumu dhidi ya Palestina

Admin.WagnerD24 Februari 2015

Mahakama ya New York, Marekani imeutia hatiani utawala wa ndani wa Wapalestina na Chama cha Ukombozi cha Palestina, PLO, kwa kuhusika na mashambulizi sita mjini Jerusalem yaliyowaua Wamarekani.

https://p.dw.com/p/1EgeF
Israel Benjamin Netanjahu Porträt 21. Dez. 2014
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin NetanyahuPicha: Reuters/A.Cohen

"Uamuzi huo unaonyesha wazi dhahiri shahiri kwamba mamlaka ya ndani ya Palestina ilikuwa na dhamana kwa umwagaji damu uliotokea muongo mmoja uliopita, na hivyo pia kuonyesha wazi kuwa hatua yake ya kutaka kujiunga na mahakama ya kimataifa ya uhalifu ya mjini The Hague, ICC, kwa lengo la kuishtaki Israel ni unafiki," amesema Netanyahu katika taarifa yake iliyotolewa saa chache baada ya hukumu kutolewa.

Netanyahu aidha amesema jumuiya ya kimataifa inapaswa kuchukua hatua za kuwaadhibu wale wanaouunga mkono na kuufadhili ugaidi na iwaunge mkono wale wanaopambana na ugaidi, katika wito wa wazi kutaka Israel iungwe mkono na ulimwengu kupinga juhudi za Palestina kujiunga na mahakama ya ICC, huku Palestina ikitarajiwa kuwa mwanachama wa mahakama hiyo kuanzia mwanzoni mwa mwezi Aprili mwaka huu.

Katika hukumu iliyotolea jana Jumatatu baraza la majaji mjini Manhattan liliipata na hatia mamlaka ya ndani ya Wapalestina na Chama cha Ukombozi cha Palestina, PLO, kwa mashambulizi sita yaliyosababisha vifo vya watu 33 na kuwajeruhi wengine zaidi ya 450 kati ya mwezi Januari 2002 na Januari 2004.

Symbolbild Israel hält palästinensische Steuergelder zurück
Rais wa mamlaka ya ndani ya Palestina, Mahmoud AbbasPicha: picture-alliance/dpa/Alaa Badarneh

Familia 10 za Wamarekani zilikwenda mahakamani kutaka kulipwa fidia kutokana na mashambulizi yaliyofanywa na kundi la Hamas na kundi la al-Aqsa Martyrs Brigades, kitengo cha kijeshi cha chama cha Fatah kilichokuwa kikioongozwa na aliyekuwa kiongozi wa Wapalestina wakati huo, hayati Yasser Arafat na baadaye kuongozwa na rais wa sasa Mahmoud Abbas.

Mahakama imeamuru PLO na mamlaka ya ndani ya Palestina ilipe fidia ya zaidi ya dola milioni 218 za Kimarekani kwa kuwapa magaidi misaada ya vifaa. Fidia hiyo inaweza kuongezwa mara tatu kwa mujibu wa sheria za kupambana na ugaidi za Marekani.

Mawakili waapa kufuatilia malipo

Wakili wa familia hizo, Kent Yalowitz amesema, "Hii ni siku muhimu kwa nchi yetu. Ni siku nzuri kwa wale wanaopambana na ugaidi. Tuna fahari na familia zetu zilizotuunga mkono. Na tumefurahishwa sana na jinsi jopo la majaji lilivyotilia maanani kazi yao. Inastaajabisha, ni uamuzi wa unyenyekevu."

Wahanga na familia zilikuwa zimeomba zilipwe zaidi ya dola milioni 350 kama fidia au zaidi ya dola bilioni moja kiwango hicho kitakapoongezwa mara tatu, kwa mashambulizi ya risasi na mabomu.

Palästina Bewaffnete Anhänger der Al-Aksa-Brigaden in West Bank
Wanachama wa Al-Aqsa BrigadesPicha: AP

Akizungumza baada ya huku kutolewa wakili wa wahanga waliodai fidia, Nitsana Darshan-Leitner alisema, "Sasa mamlaka a ndani ya Palestina inafahamu kuna gharama kwa kuwatuma washambuliaji wa mabomu wa kujitoa muhanga kuyashambulia maduka yetu makubwa, kwa migahawa yetu na kuyalipua mabasi ya abiria. Tutafuatilia na kuhakikisha mamlaka ya ndani ya Palestina inalipa kila dola kwa mujibu wa hukumu hii."

Huku Israel ikiipongeza hukumu iliyotolea, Wapalestina wameikosoa wakisema imechochewa kisiasa na viongozi wa Chama cha PLO, na mamlaka ya ndani ya Wapalestina wanatarajiwa kukata rufaa.

Kesi hiyo ilianza wiki sita zilizopita na ilikuwa ya pili katika kipindi cha chini ya mwaka mmoja ambapo jopo la majaji wa Marekani liliwatia hatiani washtakiwa kwa mujibu wa sheria ya kupambana na ugaidi, inayowaruhusu Wamarekani waliojeruhiwa na matukio ya kigaidi ya kimataifa watafute fidia katika mahakama ya shirikisho.

Mwandishi: Josephat Charo/AFP/REUTERS

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman