1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu aweka masharti ya amani

25 Mei 2011

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amesema yuko tayari kuyatoa baadhi ya maeneo ya makaazi ya walowezi kwa ajili ya amani lakini pia ametoa masharti yasiyoweza kuwarejesha Wapalestina katika meza ya majadiliano.

https://p.dw.com/p/11Nir
Benjamin Netanyahu akihutubia bunge la Marekani
Benjamin Netanyahu akihutubia bunge la MarekaniPicha: picture alliance/dpa

Netanyahu amewaambia wabunge wa Marekani hapo jana, kuwa atayaondoa baadhi ya makaazi ya walowezi wa Kiyahudi ili kuweza kupata makubaliano ya amani na Wapalestina, lakini amekataa wazo la kurejea katika mipaka ya mwaka 1967 ama kuugawa mji wa Jerusalem.

Katika hotuba yake kwa kikao cha pamoja cha Baraza la Congress, kiongozi huyo wa Israel hakupiga hatua mpya katika msimamo wake na kukataa miito muhimu kutoka kwa Rais wa Marekani, Barack Obama, pamoja na jumuiya ya kimataifa, ambao wamekuwa wakiangalia njia za kufufua hatua zilizokwama za kuleta amani.

Netanyahu pia ameondoa uwezekano wa kurejea kwenye mazungumzo wakati makubaliano ya mapatano baina ya Rais wa Palestina, Mahmoud Abbas, na kundi la Kiislamu la Hamas yanaendelea, na kuitaja hatua ya kundi hilo la Wapalestina kukataa kuitambua Israel kuwa taifa la Kiyahudi kuwa ni kikwazo kikubwa kwa amani.

"Israel inaunga mkono kwa dhati nia ya Waarabu katika eneo letu kuishi wakiwa huru. Tunataraji siku moja ambapo Israel itakuwa moja ya nchi zenye demokrasia kamili katika Mashariki ya Kati." Amesema Netanyahu.

Viongozi wa Hamas na Fatah katika mazungumzo ya kufikia maridhiano ya kisiasa
Viongozi wa Hamas na Fatah katika mazungumzo ya kufikia maridhiano ya kisiasaPicha: picture alliance/dpa

Netanyahu, ambaye hotuba yake ilikuwa ikikatizwa mara kwa mara na kushangiliwa na maseneta na wabunge wa Marekani, kwa mara nyingine tena amepinga kabisa kurejea katika mipaka iliyokuwapo mwaka 1967 kabla ya vita vya siku sita, ama kuugawa mji mtakatifu wa Jerusalem.

Suala la kukubali mipaka ya mwaka 1967 kuwa ndio sehemu ya kuanzia majadiliano limekuwa mzizi wa fitina katika mzozo unaoendelea kati ya Netanyahu na Obama.

Obama alitamka hadharani wiki iliyopita msimamo wa siku nyingi wa Marekani na jumuiya ya kimataifa kuwa taifa la Palestina linapaswa kuundwa kwa msingi wa mipaka hiyo.

Taifa hilo litajumuisha eneo la Ukanda wa Gaza, Ukingo wa Magharibi na eneo ambalo linaishi kwa wingi Waarabu la Jerusalem ya Mashariki ambayo ilitekwa na Israel, kukiwa na baadhi ya marekebisho pamoja na mabadilishano ya ardhi ili Israel iweze kuendelea kudhibiti baadhi ya makaazi ya walowezi wa Kiyahudi.

"Miaka miwili iliyopita nilisema wazi kuwa tunaunga mkono suluhisho la kuwa na mataifa mawili. Taifa la Palestina sambamba na taifa la Wayahudi. Niko tayari kufanya maamuzi magumu kufanikisha hatua hii ya kihistoria ya amani. Kama kiongozi wa Israel, ni wajibu wangu kuwaongoza watu wangu kuelekea amani. Kwa kweli si rahisi kwangu. Si rahisi, kwa sababu natambua kuwa katika amani ya kweli, tutahitajika kutoa sehemu ya ardhi ya mababu zetu." Amesema Netanyahu.

Mshauri wa Rais wa Palestina Mahmoud Abbas, Nabil Shaath, ameiita hotuba hiyo ya Netanyahu kuwa ni kutangaza vita dhidi ya Wapalestina.

"Hisia zangu ni kuwa hili si pendekezo kwa ajili ya amani. Ni matamshi zaidi juu ya vita, kulikokuzungumzia amani. Na nilifikiri kwamba mtu huyu anayetumia kila aina ya hali ya kihistoria inayokwenda kinyume na haki pamoja na nahau kadhaa kuhusu hali yetu katika ardhi yetu." Amesema Shaath.

Netanyahu amesema Israel haitatoa makaazi muhimu ya walowezi ama kuridhi masuala ya wakimbizi wa Kipalestina, na kusema mipaka ya 1967 si rahisi kuilinda.

Mwandishi: Sekione Kitojo/AFPE/Reuters
Mhariri: Abdu Mtullya