1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu ,Brown wajadiliana

25 Agosti 2009

Waziri Mkuu wa Israel na mwenyeji wake wa Uingereza wamekuwa na mazungumzo hii leo mjini London, ikiwa ni mara ya kwanza kukutana tokea Netanyahu aingia madarakani kiasi cha miezi 5 iliyopita

https://p.dw.com/p/JI4S
Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin NetanyahuPicha: AP

Mazungumzo hayo ni mwanzo wa ziara ya bwana Netanyahu barani Ulaya yenye nia ya kutuliza shutuma dhidi yake kutoka nchi za magharibi kuhusiana na ujenzi wa makaazi ya walowezi huko Jerusalem kama ni suala linalokwaza juhudi za kufufua mazungumzo ya amani ya Mashariki ya Kati.

Waziri huyo Mkuu wa Israel ambaye ni kutoka chama chenye msimamo mkali cha mrengo wa kulia,anaitumia ziara yake hiyo kujaribu kutuliza lawama za nchi za magharibi ambazo hazikubaliani na hatua ya kuendelea kujenga makaazi ya walowezi katika eneo la mashariki mwa Jerusalem.

Kitendo hicho kimekuwa kizingiti cha kuanza tena kwa mazungumzo ya amani ya mashariki ya kati, ambapo Rais wa Mamlaka ya Wapelstina Mahamoud Abbas amesisitiza kuwa ni lazima Israel isitishe ujenzi huo, kama sharti kuu la kurejea tena mezani kwa mazungumzo.

Aidha mkutano huo wa leo katika makaazi ya Waziri Mkuu wa Uingereza Downing Street, utakuwa ni nafasi kwa Netanyahu kujaribu kusawazisha uhusiano kati yake na Serikali ya Gordon Brown ambayo hivi karibuni ilisema kuwa imesikitishwa na kitendo cha kufukuzwa kwa familia mbili za kipalestina kutoka katika nyumba zao kwenye eneo la waarabu la mashariki mwa Jerusalem eneo ambalo Israel inalikalia kimabavu toka ilipoliteka katika vita vya mwaka 1967.

Bundeskanzlerin Angela Merkel
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: AP

Bwana Netanyahu pia anatarajiwa kuwa na mazungumzo na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel mjini Berlin keshokutwa Alhamisi.Ujerumani ni mshirika mkubwa kiasili wa Israel, barani Ulaya, lakini imekwishaelezea kutounga kwake mkono ujenzi wa makaazi hayo ya walowezi kwa msingi kuwa unakwanza juhudi za kufufuliwa kwa mazungumzo ya eneo hilo.

Akiwa mjini London Bwana, Netanyahu pia atakutana na mjumbe maalum wa Rais Barack Obama katika mashariki ya kati George Mitchell, ambaye amekuwa akishinikiza Israel kusitisha ujenzi wa makaazi hayo.

MAANDAMANO KUPINGA MKUTANO

Nje ya makaazi ya Waziri Mkuu wa Uingereza watu wanaopinga mazungumnzo kati ya viongozi hao wameandamana huku wakiwa na mabango yanayosomeka uhuru kwa Palestina na mhalifu wa kivita.

Netanyahu anaonekana kuwa msimamo wa kukataa shinikizo hilo, ingawaje amekubali kusitisha kwa muda utoaji vibali kwa makampuni zaidi ya ujenzi kujenga makaazi hayo.

Akizungumza kabla ya kuelekea London hapo juzi, Netanyahu alisema kuwa ana matumaini mazungumzo hayo ya amani katika mashariki ya kati huenda yakaanza tena ifikapo mwisho wa mwezi ujayo.

Afisa mmoja wa ngazi ya juu katika serikali ya Israel ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, juhudi zinaendelea kufanywa kuandaa mkutano kati ya Netanyahu, na Rais wa Palestina Mahamoud Abbas pamoja na Rais Obama pembezoni mwa kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi ujayo.

Afisa huyo amesema kuwa wana matumaini mazingira ya wakati huo yataruhusu kufanyika kwa mkutano kati ya Rais Obama ,Rais Abbas  na Waziri Mkuu Netanyahu, ikiwa ni ishara ya kuanza kwa mazungumzo ya amani ya mashariki ya kati.Serikali ya Marekani imeelezea matumaini yake kuwa mazungumzo hayo ya amani yataanza tena hivi karibuni.

  TAIFA LA PALESTINA MIAKA MIWILI IJAYO

Salam Fayyad an der Mauer in der Westbank
Waziri Mkuu wa Palelstina Salam FayyadPicha: AP

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa mamlaka ya Palestina Salam Fayyad alisisitiza haja ya Israel kusitisha kabisa ujenzi huo wa makaazi ya walowezi, ili kuyafufua mazungumzo ya amani.

Akizungumza hii leo, Bwana Fayyad alisema kuwa nchi za magharibi zinakubaliana na mipango ya kuwepo kwa taifa la Palestina katika kipindi cha miaka miwili ijayo bila ya kujali mpango wa amani.

Mwandishi.Aboubakary Liongo/AFP

Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman