1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu: Nyuklia ya Iran ni hatari kwa dunia

Admin.WagnerD28 Septemba 2012

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameionya dunia dhidi ya kitisho cha mpango wa nyuklia wa Iran.

https://p.dw.com/p/16Grw
Benjamin NetanjahuPicha: Getty Images

Netanyahu amechora mstari mwekundu kwenye umbo la bomu kuuonyesha umma uliohudhuria mkutano wa kila mwaka wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, ni kwa namna gani Iran inahatarisha amani ya dunia na huenda nchi hiyo ikaanza kuwa na silaha za nyuklia katika kipindi kisichozidi mwaka mmoja.

Netanyahu ameuambia mkutano huo kwamba njia pekee ya kuizuia Iran kutengeneza silaha za atomiki ni kuukomesha mpango wake wa Nyuklia hivi sasa. Netanyahu ameongeza kuwa mstari huo mwekundu ni muhimu ukachorwa kwa uwazi kabisa ili kuzuia vita.

Huku akisisitiza kuwa Israel na Marekani zinaweza kuchukua njia moja dhidi ya mapango wa nyuklia wa Iran. Marekani imesita kutoa matakwa ya kuwepo muda maalumu wa kuchukua hatua dhidi ya mpango huo, lakini mawaziri wa mambo ya nje wa mataifa yenye nguvu duniani wamekutana baada ya hotuba ya Netanyahu na kutoa wito kwa Iran kuwajibika haraka kwa kujibu kuhusu wasiwasi walionao dhidi ya mpango wa nyuklia wa nchi hiyo.

Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Israel akionyesha hatari ya nyuklia ya Iran
Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Israel akionyesha hatari ya nyuklia ya IranPicha: Getty Images

Kiongozi huyo amesema na hapa ninamnukuu "Hadi kufikia msimu ujao wa kipupwe karibu kabisa na majira ya joto kwa kutumia kiwango cha sasa cha urutubishaji watakuwa wamemaliza mchakato wa kati wa kurutubisha na kusonga mbele na kwenye hatua za mwisho za kutengeneza silaha za nyuklia".

Amedai kuwa Iran iko katika kiwango cha asilimia 70 ya urutubishaji wa madini ya Uranium unaofaa kutengeneza silaha za nyuklia na kutumia kalamu yake ya wino mwekundu kuchora mstari wa juu kabisa wa asilimia 90 katika kitufe chake kinachofanana na bomu na kusema kuwa hicho ndicho kiwango kisichovumilika.

Ingawa hakutishia kuishambulia Iran lakini alisema kuwa urutubishaji wa madini ya Uranium unaofanywa na nchi hiyo utaendelea kuwa kuwindwa hadi hapo katikati ya mwaka kesho ambapo anahofu kuwa ndiyo wakati ambao madini hayo yanayodaiwa kuwa ni kwa matumizi ya nishati yatakapopelekwa maabara na kugeuzwa mabomu madogo madogo.

Kauli ya Iran na Palestina

Nayo Iran imetuma mjumbe kwenye mkutano huo ikionya kwamba itajibu kwa nguvu zake zote mashambulizi yoyote dhidi yake na kuitaka jumuiya ya kimataifa kuiwekea shinikizo Israel ili kukomesha tabia yake isiyofaa.

Rais Mohmoud Ahmadinejad wa Iran
Rais Mohmoud Ahmadinejad wa IranPicha: AP

Naibu balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa Eshagh al-Habib alielezea haki ya nchi yake kujibu na kuiita Israel kuwa ni taifa linaloegemea katika ugaidi na kwamba ndio mwanzilishi wa vitendo vya ugaidi dhidi ya mataifa duniani.

Serikali ya Iran imesema inarutubisha madini ya Uranium kwa kiasi cha asilimia 20 tu cha matumizi ya kawaida.

Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya ndani Palestina
Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya ndani PalestinaPicha: AFP/Getty Images

Katika kikao cha jana Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas naye alizungumza na kusema kuwa anataka kupandishwa hadhi ya nchi yake katika Umoja wa Mataifa nchi yenye mamlaka kamili. Abbas pia alionya kwamba upanuzi wa makaazi ya walowezi uliimanisha muda wa kuwa na suluhu ya mataifa mawili umeshamalizika.

Mwandishi: Stumai George/AFP/Reuters

Mhariri: Josephat Charo