1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu ziarani Umoja wa Ulaya kuhusu Jerusalem

Sylvia Mwehozi
11 Desemba 2017

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema kwamba suala la kuitambua Jerusalem kama mji mkuu wa Isarel, litawezesha upatikanaji amani. Matamshi yake yamekuja baada ya ulimwengu kukemea hatua ya rais Donald Trump .

https://p.dw.com/p/2p8I1
Belgien Brüssel Netanyahu trifft Mogherini
Picha: Reuters/F. Lenoir

Tangazo la rais Donald Trump alilolitoa wiki iliyopita limezusha maandamano na vurugu katika mamlaka ya Wapalestina, pamoja na maandamano kadhaa katika nchi nyingi za kiislamu. Umoja wa Ulaya umetoa angalizo juu ya uamuzi huo, ambao unahitimisha sera ya miongo saba ya Marekani juu ya mgogoro wa mji mtakatifu unaozozaniwa na mawaziri wa kigeni wa Umoja huo wanatarajiwa kumtaka Netanyahu kuanzisha tena majadiliano na Wapalestina wakati anapokutana nao asubuhi ya leo mjini Brussels.

Waziri huyo mkuu wa Israel amesema alichokifanya Trump "ni kuweka ukweli mezani" kwa kutambua kuwa Jerusalem imekuwa ni mji mkuu wa Israel kwa miaka 70 na pia kwa wayahudi kwa miaka 3000. Katika taarifa yake aliyoitoa pembeni mwa mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Fedirica Mogherini, Netanyahu amesema kuwa mpango wa amani wa Marekani ndio suluhu pekee ya kusonga mbele. "Kuna jitihada sasa zinazoendelea kuleta mapendekezo mapya ya amani na utawala wa Marekani. Nadhani tunapaswa kutoa nafasi ya amani. Nadhani tunapaswa kuona kile kinachowasilishwa na kuona kama tunaweza kuendeleza amani hii," amesema Netanyahu.

Frankreich Paris Emmanuel Macron und Benjamin Netanjahu
Benjamin Netanyahu na rais wa Ufaransa Emmanuel MacronPicha: picture-alliance/abaca/C. Liewig

Mogherini ambaye alionya wiki iliyopita kuwa uamuzi wa Jerusalem unaweza kurejesha hali nyuma katika kiza kinene, amerudia msimamo wa Umoja wa Ulaya kuwa ni ufumbuzi wa mataifa mawili yani Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel na mamlaka ya Palestina na kuwa hiyo ndio njia pekee na ya kudumu ya utatuzi wa mgogoro huo."Tunaamini kuwa suluhisho pekee la mgogoro kati ya Israeli na Palestina linatokana na mataifa mawili kwa Jerusalem kama mji mkuu wa nchi zote za Israeli na mamlaka ya Palestina. Huu ni msimamo wetu na tutaendelea kuheshimu makubaliano ya kimataifa juu ya Jerusalem mpaka hatua za mwisho za jiji pekee na ufumbuzi wa moja kwa moja wa mazungumzo kati ya pande  zote na tunaamini kwamba pande zote zitashiriki moja kwa moja katika mazungumzo yenye tija kwa kuungwa mkono na  jumuiya ya kimataifa," amesema Mogherini.

Deutschland Berlin Proteste gegen US-Entscheidung zu Jerusalem
Maandamano mjini Berlin ya kupinga uamuzi wa Donald TrumpPicha: picture-alliance/abaca/E. Basay

Ziara ya Netanyahu mjini Brussels inafanyika  baada ya kukutana na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron mjini Paris hapo jana Jumapili ambapo Macron alimtaka kusimamisha ujenzi wa makazi ya kudumu na kuwashirikisha tena Wapalestina.

Naye waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Thomas de Maiziere amelaani kitendo cha uchomaji wa bendera za Israel wakati wa maandamano ya kuunga mkono Palestina mjini Berlin, akisema kwamba Ujerumani imekuwa kwa njia moja na uhusiano na taifa la Israel na waumini wa kiyahudi. Bendera mbili za Israel zilichomwa moto katika maandamano siku ya Ijumaa.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP/DPA

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman