1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NEW YORK : Ki-moon kulipa umuhimu ongezeko la ujoto

2 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCNL

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon wakati akitowa ahadi ya kuliwekea nadhari suala la kuongezeka kwa kiwango cha ujoto duniani katika mazungumzo na viongozi wa dunia hapo mwezi wa Juni amesema mabadiliko ya hali ya hewa yanatowa tishio kubwa kwa dunia sawa na vita.

Ban amesema ataweka sisitizo juu ya tatizo hilo la mabadiliko ya hali ya hewa katika mkutano nchini Ujerumani na viongozi wa nchi za kundi la mataifa manane yenye maendeleo ya viwanda duniani ambazo ni Canada,Ufaransa,Ujerumani,Uingereza,Italia, Japani,Marekani na Urusi.

Hapo jana mjini Paris Ufaransa wanasayansi kutoka zaidi ya nchi 60 walianza kuadhimisha mwaka wa kimataifa wa maeneo ya ncha za kaskazini na kusini mwa dunia kwa utafiti wa maeneo hayo ya baridi kali ya Aktiki na Antaktiki wakati tahadhari ikiongezeka juu ya kuongezeka kwa kiwango cha ujoto duniani.

Mara ya mwisho Mwaka wa Kimataifa wa Maeneo ya Ncha za Kaskazini na Kusini mwa dunia uliadhimishwa hapo mwaka 1957.