1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NEW YORK : Kikosi kwa Somalia sio cha uvamizi

8 Desemba 2006
https://p.dw.com/p/CClg

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan hapo jana amesema kikosi cha kulinda amani cha kanda kinachotazamiwa kuwekwa nchini Somalia nchi iliokosa utawala wa sheria kinapaswa kuvisadikisha vikosi vya Muungano wa Mahkama za Kiislam kwamba haviendi nchini huma kama vikosi vya uvamizi.

Hapo Jumaatano Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kauli moja limeidhinisha uwekaji wa wanajeshi wa kulinda amani 8,000 kutoka Mamlaka ya Nchi saba wanachama wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Afrika IGAD.

Annan amesema anatumai nchi zitakazotuma vikosi vyao zitatafuta njia ya kuzungumza na makundi husika nchini Somalia kuwaelewesha kwamba vinakwenda nchini humo kuwasaidia kuleta utulivu,kuwasaidia watu wao na kwamba hawendi kama ni vikosi vya uvamizi wa aina yoyote ile.

Uwekaji wa vikosi hivyo vya IGAD ambavyo vitaipa nguvu serikali ya mpito inayoungwa mkono na Ethiopia unapingwa vikali na vikosi vya Kiislam ambavyo vimeuteka mji mkuu wa Mogadishu hapo mwezi wa Juni na baadae kunyakuwa karibu eneo lote la kusini mwa nchi hiyo na kati kati ya nchi ambako wameweka utawala wa sheria kali za Kiislam