1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

New York. Korea ya kaskazini yawekewa vikwazo.

15 Oktoba 2006
https://p.dw.com/p/CD2S

Baraza la usalama la umoja wa mataifa limepiga kura kwa kauli moja kuweka vikwazo vya kiuchumi na silaha dhidi ya Korea ya kaskazini kutokana na madai yake kuwa imefanya jaribio la silaha za kinuklia.

Azimio hilo , ambalo limeitaja hatua ya Korea ya kaskazini kuwa ni kitisho kwa amani ya kimataifa na usalama , inatoa nafasi kwa nchi mbali mbali kuzuwia mizigo inayokwenda na kutoka Korea ya kaskazini na kukataza biashara ya silaha , na bidhaa zisizo muhimu na linaruhusu kuzuiwa kwa fedha zilizoko nje.

Balozi wa Korea ya kaskazini katika umoja wa mataifa Pak Gil Yon , ametupilia mbali azimio hilo na kuonya dhidi ya kuiwekea nchi yake mbinyo zaidi.

Balozi wa Marekani katika umoja wa mataifa John Bolton amesema kuwa nchi yake haitakubali kuvumilia shughuli za kinuklia za Korea ya kaskazini.

Utekelezaji wa azimio hilo utategemea sana iwapo wale wanaofanya biashara na Korea ya kaskazini watakubali kutekeleza.

Wakati huo huo , Korea ya kusini imesema kuwa bado haijaweza kugundua miale ambayo si ya kawaida ambayo inaweza kuthibitisha kuwa Korea ya kaskazini imefanya jaribio hilo la silaha za kinuklia.