1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NEW YORK : Mama Migiro wa Tanzania ni Naibu Katibu Mkuu Umoja wa Mataifa

6 Januari 2007
https://p.dw.com/p/CCcz

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amemchaguwa waziri wa mambo ya nje wa Tanzania Asha-Rose Migiro kuwa naibu wake na kutimiza ahadi yake kwamba angelimchaguwa mwanamke kushika wadhifa nambari mbili katika Umoja wa Mataifa.

Ban amemwelezea Migiro kuwa ni kiongozi anayeheshimiwa sana ambaye alikuwa akiyatetea mataifa yanayoendelea na kuonyesha umahiri wa uongozi wa kupigiwa mfano.

Ban amesema anakusudia kukasimu sehemu kubwa ya shughuli za uogozi na utawala,masuala ya uchumi jamii na maendeleo kwa mama Migiro.

Ban amemjulisha Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania juu ya uteuzi huo ambaye ameufurahia na kujivunia.

Dr. Migiro mwenye umri wa miaka 50 aliwahi kuwa mhadhiri mwandamizi katika Kitivo cha Sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,waziri wa maendeleo ya jamii,jinsia na watoto kabla ya kuchaguliwa kushika wadhifa wa waziri wa mambo ya nje wa Tanzania hapo mwezi wa Januari mwaka 2006.

Migiro ambaye ana shahada ya sheria ya Chuo Kikuu cha Dae es Salaama na ile ya udaktari katika sheria ya Chuo Kikuu cha Konstanz nchini Ujerumani anakuwa mwanamke wa pili kushika wadhifa huo katika kipindi cha miaka 10 iliopita.

Louise Frechette wa Canada alitumikia wadhifa huo kama naibu katibu mkuu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan takriban katika vipindi vyake vyote viwili vya miaka mitano mitano viliomalizika hapo tarehe 31 mwezi wa Desemba.