1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NEW YORK: Serikali ya Palestina yatakiwa kuitambua Israil.

10 Februari 2007
https://p.dw.com/p/CCTS

Kundi la pande nne linaloshughulikia amani ya mashariki ya kati limerejea wito wake kwamba serikali yoyote ya Wapalestina inapaswa kupinga matumizi ya nguvu na pia kuitambua Israil.

Hata hivyo kundi hilo limekataa kuelezea iwapo mwafaka wa kugawana madaraka umetimiza masharti yaliyowekewa Mamlaka ya Wapalestina ili kurejeshewa misaada.

Kundi hilo mapema liliipongeza Saudi Arabia kwa kuratibu mashauriano hadi ya makundi hasimu ya Wapalestina kukubaliana, mjini Makkah, siku ya Alhamisi iliyopita.

Mwafaka huo una lengo la kumaliza uhasama kati ya wafuasi wa vyama vya Hamas na Fatah na pia kuajribu kuyashawishi mataifa ya magharibi kurejesha misaada iliyosimamishwa kutokana na msimamo wa serikali ya Hamas wa kutoitambua Israil.

Uhasama kati ya chama cha Hamas na chama cha Fatah kinachoongozwa na Rais wa Palestina Mahmoud Abbas, uliongezeka mwaka uliopita baada ya Hamas kushinda uchaguzi wa bunge.

Ushindi huo wa Hamas ulisababisha mgawanyiko kwenye serikali na ghasia za mabarabarani zilizosababisha vifo vya watu zaidi ya mia moja na thelathini katika eneo la Gaza.

Chama cha Hamas kimesema kitaendelea na msimamo wake wa kutoitambua Israil.