1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NEW YORK: Sudan yatuma barua ya onyo kuhusu Darfur

6 Oktoba 2006
https://p.dw.com/p/CD5m

Umoja wa Mataifa umeonywa vikali na Sudan kuhusu mpango wa kutaka kupeleka vikosi vya amani katika jimbo la mgogoro la Darfur.Katika barua iliyopelekwa kwa madola ambayo huenda yakachangia vikosi hivyo,serikali ya Sudan imeonya kuwa hatua ya kutuma vikosi itatazamwa kama ni “kitendo cha uadui” na “mwanzo wa uvamizi.”Kufuatia barua hiyo,Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeitisha mkutano wa dharura.Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa,John Bolton ameituhumu Sudan kupinga moja kwa moja mamlaka ya Umoja wa Mataifa na kuongezea kusema kuwa kitendo cha kuandika barua kama hiyo hakijawahi kutokea. Wanajeshi 7,000 kutoka nchi za Umoja wa Afrika, wameshindwa kuzuia mapambano kati ya waasi na wanamgambo wanaoungwa mkono na serikali ya Sudan katika jimbo la Darfur,magharibi mwa nchi hiyo.Tangu mapigano kuanza mwaka 2003,kama watu 200,000 wamefariki na wengine milioni mbili wamelazimika kukimbia makwao.