1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NEW YORK:Mjumbe maalum wa UM awasilisha ripoti kuhusu Myanmar

5 Oktoba 2007
https://p.dw.com/p/C7IE

Katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki Moon amesema ameikaribisha hatua ya kiongozi wa kijeshi wa Myanmar jenerali Than Shwe kwamba yuko tayari kukutana na kiongozi anaetetea demokrasia aliye kizuizini bibi Aung San Suu Kyi.

Katibu mkuu ameyasema hayo katika mkutano wa baraza la usalama la umoja wa mataifa ambao umeitishwa kwa ajili ya kuipokea taarifa ya mjumbe maalum wa Umoja wa mataifa Ibrahim Gambari juu ya ziara yake ya siku nne nchini Myanmar.

Katika ripoti yake bwana Gambari amesema maandamano dhidi ya serikali ya Myanmar ni kilio cha umma kutokana na ukandamizaji.

Bwana Gambari ameonya kuwa hali nchini Myanmar inaweza kuleta madhara makubwa kimataifa.

Jenerali Than Shwe amesema atakutana na bibi Suu Kyi lakini kwa sharti kwamba ataacha mwito wake wa kuihimiza jamii ya kimataifa kuuwekea vikwazo utawala wa kijeshi wa Myanmar.