1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ni ama Manchester United au Chelsea leo hii

Liongo, Aboubakary Jumaa21 Mei 2008

Katika ulimwengu wa spoti leo hii hadithi ni moja tu nayo ni fainali ya ligi ya mabingwa barani ulaya kati ya Chelsea na Manchester United zote za Uingereza.

https://p.dw.com/p/E3gO
Polisi wa Urusi eneo ambalo watakaa washabiki wa soka katika eneo liitwalo Red Square mjini Moscow,wakati wa fainali ya leo kati ya Chelsea na Manchester UnitedPicha: AP

Macho na masikio ya washabiki na wasiyo washabiki wa soka yataelekezwa mjini Moscow nchini Urusi katika muda wa saa zipatazo  nane kutoka sasa.


Nyasi za uwanja wa Luzhniki mjini Moscow ziko tayari kuhimili madaluga 22 ya wachezaji wa Manchester United na Chelsea.


Wachezaji hao hivi sasa wanapiga jaramba huku washabiki wao kwa upande mwengine wakinoa makoo yao tayari kuingia uwanjani kwa mpambano huo unaosubiriwa kwa hamu kubwa.


Makocha wa timu zote mbili wana vikosi imara,ingawaje Chelsea inakabiliwa na majeruhi ambapo beki wake wa kushoto Ashley Cole aliumia wakati wa mazoezi lakini hata hivyo kocha wake Avram Grant ana matumaini atakuwa fiti leo hii kumzuia Ronaldo na wenzie.


Hii ni mara ya kwanza kwa Chelsea kufika fainali ya ligi ya mabingwa, ingwaje wamewahi kushinda mara mbili ubingwa wa kombe la UEFA.


Kwa mantiki hiyo, njaa ya kushinda kombe hilo,ni kubwa kama alivyothibitsha kiungo mshambuliaji wa timu hiyo Frank Lampard.


Mtizamo huo ndiyo waliyonao washabiki wengi wa soka huko Uingereza ya kwamba Chelsea haitakubali ikitiliwa maanani kuwa ni wiki mbili zilizopita imeshuhudia Man ikiwashinda mbio na kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya Uingereza.


Salehe Mkomoro ni mmoja wa washabiki hao anayeishi  katika mji wa Leisecter nchini Uingereza ambaye anasema kuwa Chelsea wako fiti haswa katika kiungo.


Sir Alex Ferguson kwa upande wake anajiwinda kurejea historia ya mwaka  1999 pale alipoiongoza Manchester United kushinda vikombe viwili, kile cha ligi kuu ya Uingereza na Ulaya.


Lakini zaidi anasema kutimiza miaka 50 toka ajali ya ndege iliyouwa wachezaji wa timu hiyo mjini Munich, ni hamasa kubwa ya ushindi kwao.


Sir Ferguson anajinasibu kuwa kikosi chake hivi sasa kimesheheni wachezaji imara na ana tatizo la kupanga timu kwani kila mchezaji yuko fiti.Lakini anaamini kuwa mmoja wa wachezaji atakayeingia kutokea benchi ataipatia timu hiyo ushindi kama ilivyokuwa mwaka huo wa 1999.


Katika mwaka huo  Teddy Sheringham na Ole Gunna Solskjaer waliyotokea benchi na kupachika mabao 2 dhidi ya moja la Bayern Munich iliyokuwa ikiongoza hadi wakati wa dakika za majeruhi.


Hata hivyo kwa Salehe Mkomoro, bado Ferguson ana kazi ya kuthibiti eneo la katikati kwani Chelsea wana wachezajia mahiri zaidi.


Maelfu ya washabiki  kutoka Uingereza wanamiminika jijini Moscow na wengine toka juzi wamekwishawasili katika mji huo ambao unatarajia faida ya paundi millioni 30 kwa kufanyika kwa fainali hiyo.


Inakadiriwa ya kwamba kila mshabiki kutoka uingereza atatumia kiasi cha paundi 624 mjini Moscow.


Zaidi ya watu millioni 20 watashuhudia pambano hilo nchini Uingereza huku zaidi ya millioni 100 kote duniani wakielekeza macho yao mjini Moscow.