1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ni Ivory Coast na Togo AFCON 2013

22 Januari 2013

Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2013 zinaendelea nchini Afrika ya Kusini ambapo leo (22.1.2013) vijana machahari wanaokonga nyoyo za wapenzi wengi wa kandanda barani Afrika Ivory Coast watachuana na Togo.

https://p.dw.com/p/17PUO
Ivory Coast's National football team 'Elephant' players pose for a photo before the African Cup of Nations qualification match between Ivory Coast and Senegal at the Felix Houphouet-Boigny stadium in Abidjan on September 8, 2012. AFP PHOTO / ISSOUF SANOGO (Photo credit should read ISSOUF SANOGO/AFP/GettyImages)
Bildergalerie Africa Cup Of Nations ElfenbeinküstePicha: gettyimages/AFP

Mechi hiyo ya Kundi D itachezwa kwenye uwanja wa "Royal Bafokeng Sports Palece". Ivory Coast itatinga uwanjani ikiwa na wachezaji wake wanaong'ara kwenye kandanda la kimataifa akiwemo Didier Drogba, makaka wawili wa Toure yaani Yahya na nduguye Kolo.

Kwa upande wake Togo itaingia uwanjani ikiwa na majina maarufu kama vile Emannuel Adebayor, Vincent Bossou pamoja na Dare Nibome. Mchezo huo unatarajiwa kuvuta hisia za wapenzi wa kandanda kutokana na umaarufu pamoja na historia za ubabe wa nchi hizo kwenye soka. Mchezo mwingine wa kundi D ni ule ambao wana wa Afrika ya kaskazini wataumana katika mechi inayoikutanisha Tunisia na Algeria.

Wakiwa wameshiriki fainali tano mfululizo kwa mafanikio makubwa, Drogba na wenzake wamekuwa wakiliwania taji hilo kwa udi na uvumba bila mafanikio. Timu hiyo iliyo na kiwango cha juu cha soka haijapoteza mchezo katika mechi za kawaida tangu mwaka 2010 ilipocheza mechi ya kirafiki na Poland. Katika fainali zilizopita, Ivory Coast ilikosa kombe chupuchupu kutokana na mkwaju wa penalti wa Zambia.

Didier Drogba katika moja ya mechi za timu yake ya taifa Ivory Coast
Didier Drogba katika moja ya mechi za timu yake ya taifa Ivory CoastPicha: AP

Wenyeji wahaha kusaka kombe

Nao wenyeji wa mashindano hayo Afrika Kusini wanatajwa kuwa katika hekaheka za kurekebisha kikosi chake ili kuweza kulibakisha nyumbani kombe hilo. Baada ya kuonyesha kusuasua katika mechi ya ufunguzi, vijana hao wa Bafana Bafana wanapangwa vizuri kwa ajili ya mchezo wa kundi A baina ya timu hiyo dhidi ya Angola Jumatano (23.1.2013) mjini Durban kwenye uwanja wa Moses Mabhida.

Habari kutoka kambi ya Bafana Bafana zinasema kuwa mchezaji Dean Furman anayecheza soka katika timu ya daraja la Ligi ya soka ya England aturudishwa kwenye nafasi ya kiungo wa kati ambayo katika mchezo uliopita ilikaliwa na Kagisho Dikgacoi ambaye pia anacheza ligi ya England daraja la tatu.

Waafrika kusini wengi wangependa kumuona tena mchezaji wa kati Siphiwe Tshabalala ambaye ametupwa pembeni. Tshabalala alipata bao matata katika mechi ya ufunguzi ya Fainali za Kombe za Dunia mwaka 2010 nchini Afrika Kusini na hivyo kuwavutia mashabiki wengi.

Kikosi cha taifa cha Afrika Kusini
Kikosi cha taifa cha Afrika KusiniPicha: gettyimages

Kundi A linalowahusisha wenyeji Afrika Kusini, Angola, mabingwa wa zamani wa kombe hilo Morocco pamoja na kikosi kipya katika mashindao wanavisiwani Cape Verde linakabiliwa na ushindani mkali. Cape Verde itakwaana na Morocco Jumatano (23.1.2013) katika mechi za duru ya kwanza ambayo kama watashinda basi watasonga hatua moja ya kufuzu kwa robo fainali.

Vinara wengine wa soka barani Afrika, Nigeria nao bado wanaendelea kuhangaika baada ya sare ya mchezo uliopita ya bao 1-1. Nyota wa zamani wa nchi hiyo, Sunday Oliseh, ameilaumu mikakati ya Kocha wa timu hiyo Stephen Keshi kuwa ndiyo chanzo cha matokeo hayo yenye kukatisha tamaa katika mchezo wao na Burkina Faso Jumatatu (20.1.2013) kwenye kundi C.

Oliseh, kiungo wa kati maarufu katika kikosi cha mwisho cha Nigeria kutwaa taji hilo miaka 19 iliyopita, alisema kushindwa kwa timu hiyo kulitokana na makosa yao wenyewe.

Oliseh anasema kocha Stephen anapaswa kuangalia vizuri mbinu zake za uchezaji na ni muhimu akawa na mbinu ya mtu mmoja mbele ili waweze kushinda.

Mwandishi: Stumai George/Afpe/Reuters/Dpa

Mhariri: Josephat Charo