1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ni siku ya Mdahalo Ujerumani

1 Septemba 2013

Kabla ya Wajerumani kupiga kura, wagombea wakuu wa ukansela Angela Merkel na Peer Steinbrück walipangiwa kuonyeshana makarama kwenye televisheni ukiwa ni mdahalo pekee kabla ya kufanyika kwa uchaguzi.

https://p.dw.com/p/19Zpo
Mdahalo kati ya Merkel na Steinbrück.
Mdahalo kati ya Merkel na Steinbrück.Picha: picture-alliance/dpa

Kansela Angela Merkel na mpinzani wake wa chama cha Social Demokatik Peer Steinbrück watachuana ana kwa ana katika mdahalo huo wa uchaguzi wa dakika 90 ambao utarushwa hewani moja kwa moja kwenye vituo vinne mashuhuri vya televisheni nchini Ujerumani Jumapili (01.09.2013)saa mbili na nusu usiku ambao ni wakati idadi kubwa ya watu huangalia televisheni.

Chama cha SPD kinataraji kujiongezea alama za ushindi dhidi ya Merkel anayetetea wadhifa wake kutokana na kwamba Steinbrück anaonekana kuwa ni msemaji mwenye ufasaha zaidi hadharani kuliko Merkel.

Chama cha Social Demokratik kilikuwa kikitaka kuandaliwe midahalo miwili ya televisheni kabla ya uchaguzi huo uliopangwa kufanyika tarehe 22 mwezi wa Septemba lakini serikali imesema kwamba mmoja unatosha.

Mwanachama mwandamizi wa chama hicho cha SPD Thomas Oppermann amekaririwa akiliambia shirika la habari la Ujerumani dpa " Bibi Merkel inaonyesha wazi kuwa anaogopa venginevyo asingelikataa mdahalo wa pili wa televisheni." Ameongeza kusema kwamba mpambano huo hautokuwa tafrija ya kunywa chai na kwamba Steinbrück atazungumza kwa uwazi ambapo kwa mara ya kwanza Merkel hatoweza kubabaisha kwa kukwepa masuala muhimu. Upinzani mara nyingi umekuwa ukijaribu kumuelezea Merkel kwamba ni mtu asiekuwa na hoja ambapo Steinbrück mwanzoni mwa kampeni alimshutumu kwa kuzungumza kwa kutumia "mafumbo ya bisi".

Uchunguzi wa maoni : Merkel anaongoza

Uchunguzi wa maoni hivi sasa unaonyesha kuwepo kwa matokeo mazuri ya uchaguzi kwa chama cha Merkel cha Christian Demokratik (CDU), juu ya kwamba haifahamiki iwapo mshirika wao mdogo katika serikali ya mseto chama cha kiliberali cha Free Demokratik(FDP) kitaweza kujipatia kura za kutosha kuendelea kuwa turufu ya kuunda serikali ya mseto. Mtu katika kila kundi la washiriki watatu wa uchunguzi huo wa maoni uliochapishwa na gazeti la "Bild" mwishoni wa juma wamesema kura zao kwa kiasi kikubwa zitategemea ushawishi wa mdahalo wa Jumapili.Wengi waliofanyiwa uchunguzi huo wa maoni hawakubaliani na maoni ya Opperman na chama chake cha SPD: Asilimia 62 wanatarajia Merkel atashinda vita hivyo vya maneno,wakati asilimia 16 tu imemuunga mkono Steinbrück.

SPD ilishinda mdahalo Merkel akashinda uchaguzi

Mdahalo huo umekuwepo katika muundo wake huo wa sasa wa mpambano wa ana kwa ana kati ya vyama vikuu viwili vya kisiasa nchini Ujerumani tokea mwaka 2002. Mdahalo huo wa wagombea wawili ulichukuwa nafasi wa midahalo ya meza ya duara ambayo ilikuwa ikijumuisha vyama vikuu vyote mwishoni mwa karne ya ishirini.

Angela Merkel na Gerhard Schröder katika mdahalo wa 2005.
Angela Merkel na Gerhard Schröder katika mdahalo wa 2005.Picha: picture-alliance/dpa

Kulikuwa hakuna kansela wa Ujerumani alieko madarakani kutoka vyama vyote viwili aliekubali kushiriki mdahalo wa aina hiyo hadi pale Gerhard Schröeder alipokubali kufanya hivyo hapo mwaka 2002.Schröeder ambaye anatambuliwa fika kwa ufasaha wake wa kuzungumza alikuwa nyuma kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni lakini uamuzi wake wa kupambana katika mdahalo huo na mgombea wa chama cha CDU Edmund Stoiber hatimae ulizaa matunda.

Schröeder akiwa tena nyuma kabla ya uchaguzi kwa kiasi kikubwa alihesabika kuwa mshindi tena katika mdahalo wa uchaguzi dhidi ya Merkel hapo mwaka 2005.Alipiga hatua kubwa baada ya mdahalo huo wa televisheni lakini haukutosha kumpa ushindi katika siku ya uchaguzi.

Katika vituo vinne vitakvyorusha mdahalo huo kila kituo kitatowa mtangazaji mmoja wa kuuliza masuali na kutumika kama muamuzi. Waandishi watatu mahiri - Anne Will wa kituo cha ARD, Maybrit Illner wa ZDF na Peter Kloeppel wa RTL wanaunda jopo la waandishi hao sambamba na mtangazaji tata Stefan Raab wa onyesho la michezo la watu mashuhuri katika kituo cha ProSieben.

Wapiga kura watakiwa kujitokeza kwa wingi

Rais Joachim Gauck wa Ujerumani kwa upande wake amewahimiza wapiga kura kuangalia mdahalo kwa wingi kadri inavyowezekana na kujitokeza kwa wingi siku yenyewe ya uchaguzi wiki tatu baadae.

Rais Joachim Gauck wa Ujerumani.
Rais Joachim Gauck wa Ujerumani.Picha: picture-alliance/dpa

Gauck amesema kutojali na kutokuwepo kwa utashi wa wapiga kura kunapaswa kuwa ni jambo la aina yake katika jamii kama Ujerumani. Amesema "Iwapo huna mgombea unayempenda hasa, basi angalau mpigie kura yule ambaye humchukii sana."

Mdahalo huo wa dakika 90 utagawiwa katika sehemu tano,ambapo kila sehemu itakuwa na mada tafauti. Syria matatizo ya mzozo wa madeni katika kanda ya sarafu ya euro suala la kodi na sera za kijamii ni masuala yanayotegemewa kuhodhi agenda juu ya kwamba kwa kawaida mada zinakuwa hazitangazwi hadharani kabla ya mdahalo. Kila mzungumzaji ana kati ya sekunde 60 hadi 90 kutowa majibu yao halikadhalika fursa ya kutowa kauli ya kufunga mdahalo.

Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP,dpa,Reuters)

Mhariri: Ssessanga,Iddi Ismail