1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ni upi mustakabali wa Wenger?

Bruce Amani
20 Machi 2017

Mambo sio mazuri sana kwa klabu ya Arsenal na hasa kwa mkufunzi Arsene Wenger ambaye anakabiliwa na shinikizo kutoka kila upande la kumtaka abwage manyanga.

https://p.dw.com/p/2ZZLP
Arsenal Coach Arsene Wenger
Picha: Reuters/H. McKay

Magazeti ya Daily Telegraph na Daily Mirror yamesema Wenger ataifahamisha bodi ya usimamizi ya Arsenal kuwa anataka kuurefusha mkataba wake, ambao utakamilika mwishoni mwa msimu huu. Na hata kocha wa West Bromwich Albion Tony Pulis alisema Wenger alimwambia kuwa anapania kubakia Emirates baada ya kichapo cha Arsenal cha 3-1 dhidi ya Albion.

Baadhi ya mashabiki walibeba mabango ya kumtaka aondoke lakini akizunguza baada ya mechi hiyo Wenger alisema ameshafanya uamuzi kuhusu mustakabali wake na atatangaza hivi karibuni "mtaona. Leo sina wasiwasi kuhusu hilo. Tupo katika wakati mgumu sana ambao hatujawahi kuwa nao katika miaka 20. Kwa sasa tunapoteza mechi baada ya nyingine na hilo kwangu ni muhimu kuliko mustakabali wangu

Na vipi kuhusu hisia zake kutokana na mashabiki wanaomzomea uwanjani? "Mimi huangalia mechi, siwangaalii mashabiki wakati mchuano ukiendelea. Naamini tunapaswa kukubali hilo. Unapaswa kufanya kazi yako, bila kujali wanachofikiria watu"

Arsenal haijatoa tamko lolote kuhusiana na ripoti za mustakabali wa Wenger. Hata hivyo klabu hiyo imekanusha ripoti za gazeti la leo la hapa Ujerumani – Bild kuwa wamewasiliana na kocha wa Borussia Dortmund Thomas Tuchel kuhusu uwezekano wa kuchukua nafasi ya Wenger.

Wenger alishinda mataji saba katika misimu yake tisa ya kwanza akiwa Arsenal lakini amesninda vikombe viwili tu vya FA katika miaka 12 tangu wakati huo.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Mohammed Abdulrahman