1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nigeria yaandaa mkutano kuijadili Boko Haram

14 Mei 2016

Nigeria leo Jumamosi (14.05.2016) inakuwa mwenyeji wa mazungumzo kuhusu kundi la Boko Haram pamoja na mataifa ya kanda hiyo na mataifa ya magharibi.

https://p.dw.com/p/1Injg
Nigeria Präsident Muhammadu Buhari und Paul Biya aus Kamerun
Rais Buhari wa Nigeria (katikati) akimkaribisha rais Paul Biya wa CameroonPicha: DW/Abuja

Mkutano huo umeitishwa kwa matumaini ya kuwa na ushirikiano wa karibu wa kijeshi na kusaidia kupambana na mzozo huo unaokaribia kuleta maafa ya kiutu.

Viongozi wa Benin, Cameroon , Chad na Niger wanatarajiwa kuhudhuria , pamoja na rais wa Ufaransa Francois Hollande , naibu waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Antony Blinken na waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza Philip Hammond.

Libanon Hollande trifft Tammam Salam in Beirut
Rais wa Ufaransa Francois Hollande (kushoto)Picha: picture-alliance/dpa/W. Hamzeh

Wajumbe kutoka mataifa ya Afrika magharibi na kati, pamoja na Umoja wa Ulaya pia wamealikwa katika mkutano huo.

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari , ambae ameapa kulisambaratisha kundi la Boko Haram kabla ya kumalizika mwaka mmoja akiwa madarakani, alikuwa anatarajiwa kukutana na rais Hollande katika ikulu ya rais mjini Abuja.

Nchi zote mbili hivi karibuni zilitia saini makubaliano ya mahusiano ya karibu ya kijeshi , ikiwa ni pamoja na kubadilishana taarifa za kijasusi , na Ufaransa inataka kusaidia utekelezaji wa suluhisho la kikanda katika mapambano na wapiganaji wa Kiislamu.

Antony Blinken Sicherheitsberater USA
Naibu waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Antony BlinkenPicha: picture-alliance/dpa/R. Sachs/CNP

Mahusiano ya karibu

Ufaransa kimsingi imeelekeza nguvu zake katika makoloni yake ya zamani yanayoizunguka Nigeria na inajiona kuwa katika nafasi nzuri ya kuwa na mahusiano ya karibu zaidi na maendeleo ya muda mrefu ya kiuchumi katika kanda hiyo yenye matatizo.

Mkutano huo wa kilele --- miaka miwili baada ya wa kwanza kama huo wa viongozi wa ngazi ya juu mjini Paris --- unakuja wakati jeshi la Nigeria linaingia ndani zaidi ya ngome kuu ya kundi la Boko Haram katika msitu wa Sambisa baada ya kukamata maeneo kadhaa ya ardhi katika eneo la kaskazini mashariki.

Kuba Havana Besuch britscher Außenminister Philip Hammond mit Bruno Rodriguez
Waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza Philip HammondPicha: Getty Images/AFP/E. De La Osa

Jeshi limelieleza kundi hilo la Kiislamu kuwa limesambaratika , lakini kumekuwa na tahadhari dhidi ya matumaini kupita kiasi ya kutangaza ushindi.

Blinken amewaambia waandishi habari mjini Abuja jana Ijumaa (13.05.2016) kwamba Marekani, ambayo inarusha ndege za upelelezi zisizokuwa na rubani katika anga ya Nigeria upande wa kaskazini mashariki kutoka Cameroon , hailioni kundi la Boko Haram kuwa limeshindwa.

Lakini alikiri "wamedhoofishwa" na kudokeza kuwapo na mafungamano na Dola la Kiislamu, pamoja na ripoti kwamba waasi wa Boko Haram wanapigana pamoja na wenzao wa makundi ya jihadi nchini Libya.

Nigeria Boko Haram Anschlag
Nyumba zilizochomwa moto katika shambulio la Boko Haram katika mji wa Dalori NigeriaPicha: picture alliance/AP Photo/J. Ola

"Tunaangalia kwa karibu kuhusu mahusiano haya...hiki ni kitu ambacho tunakiangalia kwa makini kwasababu tunataka kuvunja uhusiano huu," ameongeza Blinken.

Uwekaji wa jeshi la kikanda ambalo limekuwa likisubiriwa kwa muda mrefu lenye wanajeshi 8,500 kutoka Nigeria, Benin, Cameroon , Chad na Niger linatarajiwa kuwa juu katika ajenda za mazungumzo hayo ya mjini Abuja.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe

Mhariri: Yusra Buwayhid