1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ninja Marufuku Somalia

Saumu Mwasimba9 Mei 2007

Nchini Somalia serikali imepiga marufuku wanawake kuvaa ninja kwa kile kinachodaiwa ni kwa ajili ya usalama wa taifa.

https://p.dw.com/p/CHEY
Vazi la Ninja lapigwa marufuku Somalia
Vazi la Ninja lapigwa marufuku SomaliaPicha: AP

Vikosi vya usalama nchini humo vimeanza kuwavua wanawake waliovaa ninja hizo na kuzitia moto.

Vikosi vya usalama vinawavua wanawake Ninja walizovaa kujistiri nyuso zao na kuzichoma ili kuzuia wanamgambo wakiislamu wasijifiche kwa kutumia mavazi hayo na kuingia Mogadishu kufanya mashambulio.

Amri hiyo ya kuvuliwa Ninja wanawake na kuchomwa imetolewa na Mayor mpya wa jiji la Mogadishu Mohammed Omar Dere ambaye alisema wanataka kuzuia njama mpya za wanamgambo wakiislamu ambao wanadaiwa kuvaa Ninja na kuingia tena kwenye mji huo kwa lengo la kuanza mashambulizi.

Afisa wa ngazi ya juu wa Polisi Ali Nur akizungumza na shirika la habari la Reuters mjini Mogadishu alisema kila afisa wa polisi na wanajeshi wamepewa amri ya kuwanyang’anya Ninja wanawake wanaozivaa kwa sababu mashambulizi mengi yanafanywa na watu waliovaa vazi hilo.

Baadhi ya wanamgambo wa mahakama za kiislamu wamekuwa wakikamatwa wakiwa wamevalia vazi la Ninja.Wakati wa mapigano nchini humo wanamgambo hao walikuwa wakijifanya kuwa wanawake na kuwashambulia wanajeshi.

Hata hivyo njia zinazotumika kuwavua Ninja wanawake nchini humo zimeanza kuleta wasiwasi miongoni mwa Wasomali. Wakaazi wa mjini Mogadishu wanasema wanajeshi wa serikali na polisi tangu jana wamekuwa wakiwavua Ninja wanawake kwa kutumia nguvu na kuziharibu.

Ibrahim Elmi mwandishi wa habari aliyeko mjini Mogadishu amethibitisha hali hiyo na anasema maoni yanatofautiana mjini Mogadishu juu ya hatua hii.

Hapo jana inadaiwa Ninja nyingi zilichomwa na polisi.

Baadhi ya wanawake inabidi kuwakwepa polisi ili kuepuka kuvuliwa Ninja zao.

Wanawake wengi wanasema kitendo hiki hakikubaliki lakini hawana la kufanya.

Katika kipindi cha hivi karibuni wakiungwa mkono na Ethiopia wanajeshi wa serikali ya mpito waliwatimua mjini Mogadishu wanamgambo wa mahakama za kiislamu.

Tangu wakati huo lakini wamekuwa wakikabiliwa na mashambulio ya wanamgambo hao ambapo kiasi cha watu 1300 waliuwawa tangu mwezi Februari.

Wanachojiuliza wengi nchini Somalia ni je kuwavua wanawake Ninja kutasaidia chochote kuzuia mashambulio hayo ya wanamgambo wa mahakama za kiislamu.

Mwandishi wa habari Ibrahim Elmi haamini kama hilo litasaidia.

Siku chache zilizopita serikali ilitangaza kuwapa kichapo wanamgambo wengi tu lakini bado inachukua tahadhari za kupamabana na mbinu mpya zitakazochukuliwa na wapiganaji kufanya mashambulio mingine.