1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nishati mbadala barani Afrika

2 Desemba 2009

Zimesalia siku tano kabla ya mkutano wa kilele wa hali ya hewa kuanza Copenhagen,Denmark.Moja ya mada muhimu itakayojadiliwa Copenhagen katika kikao cha kilele ni hatua za kuvipunguza viwango vya gesi ya Carbon

https://p.dw.com/p/KnZF
Mradi wa Desertec wa Jangwa la Sahara

Changamoto kubwa ni ufadhili wa miradi mikubwa ya aina hiyo.Ujerumani ina azma ya kuanzisha katika kipindi cha miaka michache mradi maalum wa nishati ya jua katika jangwa la Sahara.Mradi huo utakaoyahusisha makampuni kadhaa utafahamika kama Desertec.Mali ni moja ya mataifa masikini ulimwenguni na ili kujikwamua inaweza kuanzisha miradi midogo ya kuzalisha nishati.

11.08.2009 DW-TV WIRTSCHAFT MINIREPORTAGE Solar
Mitambo ya kunasia miale ya juaPicha: DW-TV

Ukiitia akilini nchi ya Mali iliyo katika eneo la Sahel lililo karibu na mto Niger linakuwa na jua kali mwaka mzima.Jee kwanini mradi kama huu haujakuweko katika eneo la jangwa ambako wakazi wake wanatumia mkaa unaotengezwa na miti?.Mali ni moja ya mataifa masikini ulimwenguni na ili kujikwamua inaweza kuanzisha miradi midogo ya kuzalisha nishati. Serikali ya Ujerumani imekuwa ikiisadia nchi hiyo kufadhili miradi midogo ya kutoa nishati ya jua isiyoharibu mazingira .

Mabadiliko ya maisha

Abdoulaye anayesikiliza kiredio chake kidogo kilichounganishwa na nyaya maalum kwenye betri…muziki huo ni wa Tracy Chapman anayeyaelezea mageuzi naye anayaafiki.Maisha ya wakazi wa eneo la Quellesebougou kijijini Tiel yamekuwa na mabadiliko mengi.Awali walilazimika kupika kwa kuni,hawakuwa na umeme,barabara nzuri ila mabetri tu hayo kukuu,''Tulikuwa tukiyatumia haya mabetri kuu kuu ambayo lazima yakaongezewe nguvu mtamboni kila wakati nako ni mbali.Hali ya usalama huko nayo pia ilikuwa si nzuri na mabetri yenyewe yanaisha nguvu upesi baada ya kuyatumia kwa muda mfupi.Kwa sasa lakini tunatumia mabetri yanayotumia nishati ya jua ambayo japo yako ghali yameyafanya mambo kuwa rahisi.'' alieleza.

Taoudenni Mali Afrika Flash-Galerie
Mali iliyo katika eneo la SahelPicha: picture-alliance / united-archives/mcphoto

Abdoulaye alikuwa anafanya kazi ya kutengeneza baiskeli zilizoharibika.Mafundi wengi kama yeye waliomo kijijini mwake walilazimika kuyafunga maduka yao pindi jua linapozama kwasababu ya ukosefu wa umeme.Mambo kwa sasa yamebadilika na anaweza kuendelea na kazi yake hata usiku. Shirika linalosimamia miradi ya ushirikiano na maendeleo la GTZ limewasaidia wanakijiji wa eneo hilo kwa kuanzisha miradi iliyo na makao yake makuu huko Mali.Miradi hiyo inawalenga hasa wahandisi wanaoshirikiana na wakazi wa maeneo ya vijijini ambayo yamesahaulika kwa muda mrefu.Mhandisi wa shirika la GTZ Moussa Doumbia anaeleza,''Tumeshafanya tathmini na kukadiria kuwa tutayakidhi mahitaji ya nishati ya wakazi alfu 16….katika afisi ya Meya,shuleni,kwenye hospitali ndogo ya eneo na majumbani.Hapa tuna mitambo 12 ya kunasia miale ya jua itakayoibadili kuwa nishati.Kila mtambo unaotoa kiasi cha wati 55 za umeme umeunganishwa na betri maalum.Kwa siku tunaweza kuziongezea nguvu betri 5 za aina hiyo.''alifafanua.

Hata hivyo sio kila mwanakijiji aliye na uwezo wa kuwa na betri ya aina hiyo.Kampuni mpya ya nishati ya ELCOM inawapa wanakijiji hao mikopo iliyo na riba ya kiwango cha chini.Wengi ya wanakijiji hao wamelazimika kuungana pamoja ndipo waweze kuipata huduma hiyo.Wakazi wengi wameweza kuwa na televisheni za kisasa na kwa jumla maisha yao yameimarika.Watoto nao wamelifurahia darasa jipya lililojengwa ambalo lina taa inayotumia nishati ya jua.

Demokrasia imeimarika

Mbali ya yote hayo hali ya usalama imeimarika kijijini humo kwani kuna mwanga mchana kutwa na kwa muda mrefu zaidi wakati wa usiku.Barabara za eneo hilo kwa sasa zina taa ambazo zinatumia nishati ya jua jambo linalompa sifa meya wa mji.Yote hayo yamechangia pia katika kuimarisha demokrasia wakati wa uchaguzi wa majimbo kwani kura ziliweza kuhesabiwa kukiwa na mwanga.Kimsingi nishati ya jua ambayo haiyaharibu mazingira inaimarisha demokrasia katika kijiji hicho kidogo cha Mali kwasababu ya mradi ulioanzishwa na Shirika la GTZ la Ujerumani.Hilo huenda likaliwezesha eneo hilo kutimiza lengo la kuvipunguza viwango vya gesi ya Carbon jambo ambalo halingeweza kufanyika!


Mwandishi:Thelma Mwadzaya-ZPR/Alexander Göbel

Mhariri:Abdul-Rahman