1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gaza Israel

Oumilkher Hamidou19 Januari 2009

Kila la kufanya lifanywe kuzuwia vita visiripuke tena Gaza

https://p.dw.com/p/GbdD
Vita GazaPicha: AP


Israel imeanza kuwarejesha nyuma wanajeshi wake toka ukanda wa Gaza.Kila upande,Israel na Hamas,unasherehekea hatua hiyo kua ni ushindi kwao.Kipi lakini cha kuangaliwa kama ushindi kutokana na kurejea nyuma wanajeshi hao wa Israel?


Baada ya vita kutulia huko Gaza,wahanga wameachwa nyuma na "washindi " wanajipeleka safu ya mbele.Na kila mmoja anajinata kua mshindi.Hali hiyo imechanganyika kidogo na tabia ya kutojali mambo ambayo mashariki ya kati ndio kwao; Waziri mkuu wa muda Ehud Olmert,sawa na mshirika wake katika serikali ya muungano,waziri wa ulinzi Ehud Barack,kila mmoja anamsifu mwenzake,kabla ya vyama vyao kuanza upya kampeni za uchaguzi zilizositishwa.Na kupitia kipaza sauti cha msikitini huko Gaza,anasikika kiongozi wa Hamas,Ismael Haniya,aliyetoka mafichoni,akidai kundi lake limeibuka na ushindi.

Wanasiasa wa Israel wanasisitiza lengo la opereshini yao limelifikiwa.Lengo hilo hasa ni lipi?Jee ni kuwateketeza Hamas?Jambo hilo halikufanikiwa kama vile ambavyo halikufanikiwa lengo la kuwateketeza Hisbollah mwaka 2006 nchini Libnan.Sasa ndio tuseme wamezuwia makombora yasiweze tena kuvurumishwa kutoka Gaza?Saa chache baada ya silaha kuwekwa chini,makombora yamefyetuliwa.Hata mtindo wa kuingiza kichini chini silaha hadi Gaza,haujakoma.Kama sivyo,kwanini basi viongozi mashuhuri wa Ulaya wamefunga safari hadi Mashariki ya kati kutaka mtindo huo ukome?


Hamas kwa upande wao wanajaribu kujionyesha kuwa wao ndio wapinzani wa kweli dhidi ya kukaliwa maeneo ya Palastina na Israel.Wapalastina wanabidi watambue kwamba ukanda wa Gaza,ingawa umekua ukisumbuliwa sana na Israel tangu Hamas waliponyakua madaraka,lakini haumo tena katika orodha ya maeneo yanayokaliwa tangu Israel ilipolihama eneo hilo mnamo mwaka 2005.Hamas sasa inatoa masharti ya kutekeleza mpango wa upande mmoja wa kuweka chini silaha:Israel inabidi ihamishe wanajeshi wake mnamo muda wa wiki moja ijayo,la sivyo....?La sivyo nini?

Vipi na nguvu gani walizo nazo Hamas kuweza kutoa vitisho kama hivyo?Ndio kusema wataanza tena kupigana?Tafsiri ya hayo walimwengu wameshaiona.Wanapinga mazungumzo ya amani pamoja na Israel.Kama Hamas wana msimamo basi ni huo.

Si serikali ya Israel na wala si Hamas,hakuna anaestahiki kuutumia mpango wa kuweka chini silaha kwa masilahi ya propaganda.Kila upande unabidi uuheshimu mpango huo bila ya masharti na kutambua sio huruma iliyopelekea silaha kuwekwa chini bali kizungumkuti cha kutojua vipi kujitoa kati hali hii.Pande zote mbili zimedhihirisha kwa mara nyengine tena,kile ambacho tangu zamani kilikua kikijulikana:Kwamba mtutu wa bunduki hausaidii kutatua ugonvi,badala yake unazidisha makali ya ugonvi.


Kichaa hicho kimepelekea zaidi ya watu elfu moja kupoteza maisha yao na maelfu kujeruhiwa na zaidi ya milioni moja na nusu wengine kuatilika.Yote hayo ili tuu watu wafikirie mustaskbal usiokua na uhakika wa kuweka chini silaha?Hasha,njia na utaratibu unabidi upatikane ili kufufua mazungumzo ya amani na kuondoa uwezekano wa kuzuka tena vita huko Gaza.Hilo lakini ni shida zaidi kulifikia kuliko kutuma madege ya kivita na vifaru au kupiga porojo.Hapo Wapalastina,licha ya tabu na mashaka yote wayaonayo,wanabidi wanyooshe mkono wa amani ,na Israel nayo inabidi ikubali kwa dhati.

Yeyote atakaejaribu kufuja juhudi hizo,anastahiki kutengwa kisiasa na kupuuzwa-hastahiki kupigiwa kura.Naiwe Israel au Palastina.