1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nuri al Maliki aahidiwa ushirikiano kuleta usalama nchini mwake.

Sekione Kitojo9 Agosti 2007

Rais Mahmoud Ahmedinejad wa Iran amemwambia waziri mkuu wa Iraq Nuri al-Maliki aliyeko katika ziara nchini Iran , kuwa nchi hizo mbili zinawajibu mkubwa wa kuleta hali ya amani na usalama katika eneo hilo.

https://p.dw.com/p/CH9p
Makamu wa kwanza wa rais wa Iran Parviz Davoodi (kulia) akiwa na waziri mkuu wa Iraq Nuri al Maliki wakati wa mapokezi.
Makamu wa kwanza wa rais wa Iran Parviz Davoodi (kulia) akiwa na waziri mkuu wa Iraq Nuri al Maliki wakati wa mapokezi.Picha: AP

Waziri mkuu wa Iraq Nuri al Maliki leo Alhamis amepewa ahadi na viongozi wa Iran ya kuunga mkono juhudi za kurejesha hali ya usalama nchini Iraq, licha ya shutuma kutoka Marekani kuwa Iran iko nyuma ya mashambulizi yanayotokea nchini humo.

Maliki ambaye anakabiliwa na matatizo kadha ya kisiasa nchini mwake alikutana na rais Mahmoud Ahmedinejad, mkuu wa usalama wa taifa Ali Larijani na maafisa wengine wa ngazi ya juu katika siku yake ya kwanza ya ziara ya siku mbili yenye lengo la kupanua zaidi uhusiano ambao unazidi kukua kati ya nchi hizo mbili.

Iran na Iraq kwa pamoja zina wajibu mkubwa wa kuleta amani na usalama katika eneo hili, Ahmedinejad amemwambia Maliki baada ya mkutano wao jana Jumatano.

Hali katika eneo hilo hivi sasa , ikiwa ni pamoja na Iraq, ni tete mno. Iran inaiona hali ya baadaye ya eneo hilo kuwa inategemea sana ushindi nchini Iraq, rais huyo ameongeza.

Tovuti ya shirika la utangazaji la Iran imesema kuwa katika mkutano na mkuu wa usalama wa taifa Ali Larijani , upande wa serikali ya Iran umeleeza kuwapo kwao tayari kuisaidia Iraq kutatua matatizo yake ya kisalama.

Mazungumzo ya Maliki yanaonekana kuthibitisha kuongezeka kwa uhusiano mzuri ambao umejitokeza baina ya Iraq yenye idadi kubwa ya waumini wa madhehebu ya Shia pamoja na Iran ambayo nayo ina Washia wengi kufuatia kuanguka kwa utawala wa Saddam Hussein wa Wasunni mwaka 2003.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Iran IRNA, Maliki ameishukuru Iran kwa kutoa mchango wake muhimu wa kuleta usalama na kupambana na magaidi nchini Iraq.

Lakini Marekani ,inaishutumu Iran kwa kuchochea ghasi ambazo zimeikumba Iraq kufuatia kuangushwa kwa Saddam Hussein. Marekani inadai kuwa Iran inaunga mkono wanamgambo wa Kishia na kuwapa silaha zinazoweza kupenya katika magari ya kijeshi ya Marekani. Madai hayo yanapingwa kwa nguvu zote na Iran.

Katika tukio la kuonyesha ishara njema , Maliki alikutana na familia za maafisa saba waliokamatwa nchini Iraq na majeshi ya Marekani kwa tuhuma za kuwa wanajeshi wa jeshi maalum la Iran wakiwa katika ujumbe wa kuleta ghasia nchini Iraq. Iran inasisitiza kuwa watu hao ni wanadiplomasia na inaonekana kuwa Marekani haijaonyesha ishara za kuwaachia huru.