1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mtaifa watoa ripoti

Sylvia Mwehozi15 Septemba 2016

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi UNHCR limetoa ripoti inayoonyesha kwamba watoto milioni 3.7 ambao ni karibu nusu ya watoto milioni sita wakimbizi duniani hawana shule za kwenda.

https://p.dw.com/p/1K2si
Griechenland Flüchtlingsunterkünfte in Lagadikia
Picha: Getty Images/AFP/S. Mitrolidis

Mkuu wa shirika hilo la UNHCR Fillipo Grandi katika taarifa yake amesema "hiyo inawakilisha mgogoro kwa mamilioni ya watoto wakimbizi" na kutoa wito kwa jitihada za kimataifa katika kuhakikisha watoto hao wanarejea shuleni.

Kauli yake inakuja kabla ya kufanyika kwa mkutano wa kilele wa kwanza na wa aina yake wa Umoja wa Mataifa kuhusu wakimbizi na wahamiaji utakaofanyika septemba 19 jijini New York na kufuatiwa na mkutano mwingine siku ya pili utakaoshuhudia utoaji wa ahadi mpya za misaada ya wakimbizi mwenyeji wake akiwa ni rais wa Marekani Barack Obama.

Grandi amesema "wakati jumuiya ya kimataifa inapotafuta njia bora ya kukabiliana na mgogoro wa wakimbizi, ni muhimu pia kufikiri zaidi ya maisha ya msingi" akiongeza kwamba kwa wastani wakimbizi huyakosa makazi yao kwa karibu miaka 20. Kwa mujibu wake, hii ni zaidi ya maisha yote ya utotoni akisema elimu inawasaidia wakimbizi kuwa na fikra chanya kuhusu mustakabali wa nchi walizopewa hifadhi na hata nchi wanakotoka ikiwa siku moja watarejea.

Mkuu wa shirika la UNHCR Filippo Grandi
Mkuu wa shirika la UNHCR Filippo GrandiPicha: picture alliance/AP Photo/S. Di Nolfi

Ripoti hiyo ya UNHCR kuhusu elimu ya wakimbizi inalinganisha na taarifa za shirika la elimu na utamaduni la Umoja wa Mataifa UNESCO juu ya uandikishwaji wa watoto katika shule kidunia,na kubainisha kwamba asilimia 50 ya watoto wakimbizi duniani kote wanapata elimu ya msingi.

Hali inakuwa ngumu zaidi watoto wanapokuwa watu wazima kwani ni asilimia 22 pekee ya watoto wanaoishi kama wakimbizi hupata elimu ya sekondari. Ripoti hiyo imesema jitihada za UNHCR na wadau wengine za kuwaandikisha watoto wakimbizi katika shule zimekuwa zikitatizika na ongezeko la idadi mpya ya watu wasiokuwa na makazi.

Zaidi ya nusu ya watoto wakimbizi duniani wasiokwenda shule wanaishi katika nchi saba: Chad, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Ethiopia ,Kenya, Lebanon, Pakistan na Uturuki. Ripoti hiyo imesema hali katika nchi iliyotawaliwa na vita ya Syria inaonyesha namna gani mgogoro unavyoweza kubadilisha mwelekeo chanya wa elimu.

Watoto wakicheza mjini Aleppo Syria
Watoto wakicheza mjini Aleppo SyriaPicha: Reuters/A. Ismail

Kabla ya taifa hilo la Syria kutumbukia katika vita ya wenyewe kwa wenyewe miaka mitano iliyopita asilimia 95 ya watoto nchini Syria walipata elimu ya msingi na sekondari. Kufikia mwezi juni mwaka huu ni asilimia 60 pekee ya watoto waliokwenda shule na kuacha idadi ya watoto milioni 2.1 wasiokwenda shule kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa. Wakati huo huo, karibu watu milioni tano wa Syria wamekimbilia nchi jirani ambako upatikanaji wa elimu umekuwa mgumu sana. Umoja wa Mataifa unakadiria watoto laki tisa wa Syria hawako shuleni.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP

Mhariri: Caro Robi