1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nyaraka za bin Laden zachapishwa

4 Mei 2012

Marekani imechapisha baadhi ya nyaraka zilizokamatwa kwenye maficho ya mwisho ya aliyekuwa kiongozi wa mtandao wa al Qaida, Osama bin Laden. Nyaraka hizo zinaionyesha al Qaida kama kundi lililozingirwa na kudhoofika.

https://p.dw.com/p/14pU6
Osama bin Laden)
Osama bin LadenPicha: AP

Nyaraka hizo ambazo ziliwekwa kwenye mtandao Alhamisi, ni sehemu ndogo tu ya zile zilizogunduliwa na Marekani, baada ya wanajeshi wake kumvamia na kumuuwa Osama bin Laden nchini Pakistan mwaka uliopita. Wamefanya makusudi, kuonyesha upande mbaya sana wa al Qaida, kwa sababu kuuawa kwa bin Laden kunachukuliwa na utawala wa Rais Barack Obama kama tukio muhimu kwa usalama wa taifa. Tukio hilo pia ni mada inayopendelewa sana na Rais Obama katika kampeni yake ya kutaka kuchaguliwa tena.

Kifo cha bin Laden, turufu ya Obama

Utawala wa Obama umekataa kuchapisha nyaraka zote za bin Laden zilizokamatwa, na hizi 17 ambazo maafisa wa Marekani wanataka ulimwengu uzione, haziwezi kutoa picha halisi ya hali ya mtandao huo wa kigaidi.

Nyumba alimouawa Osama bin Laden mjini Abbotabad Pakistan
Nyumba alimouawa Osama bin Laden mjini Abbotabad PakistanPicha: picture-alliance/dpa

Kilicho dhahiri kutokana na nyaraka hizo ni kwamba viongozi wa al Qaida wamekuwa wakikoseshwa amani na mashambulizi ya ndege za Marekani zisizo na rubani, huku wakijaribu pia kuepuka mitego ya shirika la kijasusi la Marekani CIA, na mawakala wa vyombo vingine vya usalama vya nchi hiyo.

Mchambuzi kutoka chuo kikuu cha Washington, Stephen Tunkel anasema nyaraka hizo zinaonyesha kuwa Osama bin Laden alikufa akiwa na huzuni.

''Bin Laden hakuwa mtu mwenye raha wakati wa kifo chake, tukichukulia jinsi alivyokuwa akiona mahali inakoelekea al Qaida. Nyaraka hizi zinaonyesha kuwa alikuwa na wasi wasi mkubwa na makundi yenye mafungamano na al Qaida, na jinsi asivyo na uwezo wa kuyadhibiti, na namna vitendo vya makundi hayo vilivyokuwa vikiipaka matope sura ya mtandao wake''. Amesema Tunkel.

Tamaa ya mafanikio

Katika barua moja, bin Laden au msaidizi wake anakiambia kikundi chenye uhusiano na al Qaida nchini Yemen kuwa itakuwa kazi bure kuweka madarakani serikali inayowapendelea, kwa vile Marekani ina nguvu za kuiangusha serikali yoyote watakayoiweka.

Bin Laden alionyeshwa kukatishwa tamaa na kushindwa kwa vikundi vya jihad
Bin Laden alionyeshwa kukatishwa tamaa na kushindwa kwa vikundi vya jihadPicha: picture alliance/dpa

Mara kwa mara bin Laden na watu wake wa karibu wanaonekana kuyasihi makundi ya kigaidi kuwalenga tu wamarekani, na kuacha kuwauwa waislamu wasio na hatia.

Kutoka ndani ya maficho yake nchini Pakistan, Osama bin Laden anaonekana kuelewa fika jinsi hadhi ya mtandao wake ilivyokuwa ikishuka miongoni mwa umma wa kiislamu. Katika barua aliyoiandika mwaka 2010, bin Laden anasema atatoa tangazo linaloanzisha kipindi kipya cha kukosoa makosa waliyoyafanya, kurudisha imani imano iliyopotea.

Nyaraka hizo ambazo ziliandikwa kati ya mwaka 2006 na 2010, zinaonyesha kuwa uhusiano kati ya al Qaida na Iran ulikuwa mbaya, kwa sababu Iran iliwafunga wanachama wa kundi hilo wakiwemo ndugu zake Osama bin Laden.

Msomi kutoka Chuo cha West Point cha Marekani, Nelly Godahn, anasema ujumbe muhimu uliolengwa katika kuzichapisha nyaraka hizo, ilikuwa kuonyesha kuwa bin Laden alikuwa anasumbuliwa na ukosefu wa ustadi miongoni mwa wapiganaji wa jihad wenye uhusiano na mtandao wake.

Mwandishi: Daniel Gakuba/APE

Mhariri: Oummilkheir Hamidou