1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nyati wanane wafariki baada ya kupigwa na umeme

12 Aprili 2024

Nyati wanane wamekufa hapo hapo baada ya kupigwa umeme katika mbuga ya wanyama pori ya Ziwa Nakuru nchini Kenya.

https://p.dw.com/p/4ehvb
Nyati
Nyati kadhaa wamekufa baada ya kupigwa umeme katika mbuga ya wanyama pori ya Ziwa Nakuru Kenya. Picha: Hussein Faleh/AFP/Getty Images

Tukio hilo limetokea baada ya nyati hao kugusana na nyaya za umeme uliokuwa na nguvu kubwa ambazo zilikuwa zikining'inia chini. 

Maafisa wa Shirika la huduma kwa wanyama pori nchini Kenya waliothibitisha mkasa huo wameeleza kuwa tukio hilo limesababishwa na kuvunjika na kuanguka kwa vigingi vilivyokuwa vimebeba nyaya za umeme, kutokana na mvua kubwa inayonyesha sehemu hiyo. 

Shirika hilo limechukua tahadhari na kubadilisha vizuizi hivyo vilivyokuwa vimetengenezwa kwa mbao na kuweka aina ya chuma.

Matukio ya wanyama pori kufariki kwa kupigwa na umeme yamekuwa mengi eneo hilo, na shirika la KWS limekuwa likishirikiana na shirika la umeme la nchin hiyo kuikabili hali.