1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama aanza ziara Australia

16 Novemba 2011

Rais wa Marekani Barack Obama na Waziri mkuu wa Australia Julia Gillard wametangaza mpango wa kuimarisha ushirikiano wa kijeshi kati ya nchi zao.

https://p.dw.com/p/13BLB
Rais wa Marekani Barack Obama
Rais wa Marekani Barack ObamaPicha: dapd

Rais wa Marekani Barack Obama na Waziri mkuu wa Australia Julia Gillard wametangaza mpango wa kuimarisha ushirikiano wa kijeshi kati ya nchi zao.Rais Obama ambaye yuko kwenye ziara ya siku mbili nchini Australia amesema kituo cha kwanza cha jeshi la Marekani kinaweza kufunguliwa kaskazini mwa Australia mwaka ujao. China inayoibuka kama taifa kubwa kijeshi katika eneo la Asia Pacific, imesema mpango wa Marekani na Australia haufai.

Ziara ya Obama inafanyika wakati nchi hizo zikiadhimisha miaka sitini ya ushitrikiano katika sekta ya ulinzi. Baada ya kuwasili kwake katika mji wa Canberra, Rais Obama alisema mpango wa kufungua kituo cha kijeshi kaskazini mwa Australia kinaenda sambamba na sera ya nchi yake katika eneo zima la Asia pacific.

Alisema, ''Kufungua kituo hiki cha kijeshi ni muhimu kwa sababu kutatuwezesha si kuimarisha tu ushirikiano baina ya nchi zetu mbili, bali pia tutaweza kuwasaidia marafiki zetu wengine katika eneo hili, kuwapa mafunzo na mazoezi. Na kuwepo kwetu kujeshi kutakuwa hakikisho katika mpangilio mzima wa kiusalama katika eneo''.

Maendeleo haya yanatokea wakati China, taifa lenye nguvu kubwa zaidi za kijeshi katika eneo hilo ikiwa pia inapanua ushawishi wake, na mpango wa kuwekwa kwa wanajeshi wa Marekani haukupokelewa vyema mjini Beijing.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje wa China Liu Weimin, amesema mpango huo ambao kwa mujibu wa Rais Obama utaanza kutekelezwa mwaka kesho, haufai.

''Pengine si hatua sahihi kuimarisha ushirikiano wa kijeshi na tunaamini mpango huo hauna manufaa yoyote kwa nchi za kanda hii''. Alisema Liu Weimin na Kuongeza kuwa China inapendelea ushirikiano zaidi katika masuala ya maendeleo, hususan wakati huu ambapo uchumi wa dunia unakabiliwa na changamoto kubwa.

Mpango wa Marekani kujizatiti kijeshi katika eneo la Asia Pacific unachukuliwa kama mkakati wa kutetea maslahi yake katika eneo hilo dhidi ya China ambayo nguvu zake kiuchumi na kijeshi zinaongezeka kila kukicha.

Lakini Marekani imekanusha kuwa hatua hizi zinachukuliwa kwa kuhofia nguvu hizo za China. Akiongea mjini Canberra, Rais Barack Obama amesema dhana kuwa Marekani inaiogopa China imepotoka.

Marekani imekuwa ikitiwa wasiwasi na mienendo ya China ya kujishindia maeneo mapya ambayo imezua migogoro na majirani zake. Wizara ya mambo ya nchi za nje ya China kupitia msemaji wake imesema kipaumbele kwake ni maendeleo katika mazingira ya amani, kama ilivyo matarajio ya jamii nzima ya kimataifa.

Naye waziri mkuu wa Australia Julia Gillard amesema ushirikiano wa kijeshi kati ya nchi yake na Marekani haupaswi kuchukuliwa kama kitisho kwa China.

'' Nadhani ni sahihi na jambo linalowezekana katika eneo hili la dunia linaloendelea haraka, kushirikiana na Marekani kijeshi, na kuendeleza uhusiano mwema na majirani zetu, ikiwemo China''. Alisema Gillard.

China ni mshirika mkuu wa kibiashara wa Australia, na viwanda vyake vinavyoongezeka huagiza kwa wingi mali ghafi kutoka nchi hiyo.

Ingawa hatua za Marekani kujizatiti kiulinzi katika eneo hilo ni kama ujumbe kwa China na mikakati yake ya kijeshi, Rais Barack Obama amesisitiza kuwa hawana azma ya kuitenga nchi hiyo.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFP/AP

Mhariri:Abdul-Rahman Mohammed