1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama ahudhuria mkutano wa nchi za Asia Mashariki

Josephat Nyiro Charo20 Novemba 2012

Rais wa Marekani Barack Obama amekutana leo (20.11.2012) na waziri mkuu wa China anayeondoka madarakani, Wen Jiabao, kandoni mwa mkutano wa kilele wa mataifa ya Asia Mashariki, unaonza leo Phnom Penh, Cambodia.

https://p.dw.com/p/16m5s
U.S. President Barack Obama, center, smiles as he joins a group photo with from left, Indonesia's President Susilo Bambang Yudhoyono, Brunei's Sultan Hassanal Bolkiah, Cambodia's Prime Minister Hun Sen and China's Prime Minister Wen Jiabao prior to a gala dinner in Phnom Penh, Cambodia, Monday, Nov. 19, 2012. Obama is in Cambodia on the final leg of his three-country tour of Southeast Asia. (AP Photo/Apichart Weerawong)
ASEAN Gipfel Barack Obama Wen JiabaoPicha: picture-alliance/dpa

Rais wa Marekani Barack Obama amesema uhusiano kati ya nchi yake na China ni wa ushirikiano na wa maana. Amesema kuna umuhimu mkubwa kwa mataifa hayo mawili kushirikiana kuweka msingi wa sheria ulio wazi kwa ajili ya biashara na uwekezaji.

Kwa niaba ya utawala wa China unaoondoka na ule unaojiandaa kuchukua hatamu za uongozi, Wen amempongeza Obama kwa kuchaguliwa tena kuingoza Marekani. Mkutano huo ni wa mwisho kati ya Obama na Wen ambaye anaachia ngazi pamoja na rais wa China Hu Jintao katika mageuzi ya utawala katika kipindi cha muongo mmoja.

Wakati huo huo, rais Obama amefanya mazungumzo pia na waziri mkuu wa Japan, Yoshika Noda, pembezoni mwa mkutano huo. Noda ameonya kuhusu ongezeko la wasiwasi wa kiusalama barani Asia huku kukiwa na mivutano juu ya mipaka. Kiongozi huyo wa Japan anayetarajiwa kushindwa katika uchaguzi mwezi ujao, ameipongeza sera ya kigeni ya Obama kuelekea eneo hilo, akisema uhusiano kati ya Marekani na Japan ni muhimu kuzingatia hali ya usalama mashariki mwa Asia.

Obama akabiliwa na kibarua kigumu

Rais Obama anatarajiwa leo kupiga mbizi katika maji marefu ya kidiplomasia atakapozungumzia mzozo wa bahari ya China kusini. Anatarajiwa pia kuelezea wasiwasi wake kuhusu mzozo kati ya China na majirani zake wa kusini mashariki mwa Asia, ambao umezua wasiwasi katika eneo hilo mwaka huu na kukwamisha juhudi za kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi. Akizungumza hapo jana, Wen alisisitiza kwamba mzozo huo hautakiwi kufanywa kuwa wa kimataifa na kujadiliwa kwenye mikutano mikubwa kama wa Phnom Penh.

U.S. President Barack Obama (L) meets with Chinese Premier Wen Jiabao (R) at the East Asia Summit in Phnom Penh, November 20, 2012. REUTERS/Jason Reed (CAMBODIA - Tags: POLITICS)
Rais wa Marekani, Barack Obama (kushoto) na Wen Jiabao (kulia)Picha: Reuters

China, ambayo inadai bahari yote ni himaya yake, inapendelea kufanya mashauriano ya moja kwa moja na majirani zake kutoka Jumuiya ya mataifa ya kusini mashariki mwa Asia, ASEAN, wenye wanachama 10. Rais Obama amesema anaamini kuna haja ya kupunguza wasiwasi kuhusiana na mzozo wa mipaka katika bahari ya China

Lakini kwa mujibu wa taarifa ya mwisho ya mkutano wa jana kati ya Marekani na jumuiya ya ASEAN, Obama na viongozi wa jumuiya hiyo walikubaliana kuunga mkono muongozo wa sheria wa kanda hiyo kusuluhisha mivutano juu ya mipaka.

Cambodia ni kituo cha mwisho cha ziara ya siku tatu ya Obama kusini mashariki mwa Asia baada ya kuzitembelea Myanmar na Thailand.

Mwandishi: Josephat Charo/APE/AFPE/

Mhariri: Daniel Gakuba