1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama akataa kuhusisha kutambuliwa Israel na makubaliano ya nyuklia ya Iran

Mohammed Khelef7 Aprili 2015

Rais Barack Obama ameukataa wito wa Israel kutaka makubaliano ya kinyuklia na Iran yaambatanishwe na sharti la Iran kuitambua haki ya kuwepo kwa taifa la Israel, akisema huo ni upotoshaji mkubwa.

https://p.dw.com/p/1F3TJ
Rais Barack Obama wa Marekani.
Rais Barack Obama wa Marekani.Picha: Reuters/M. Theiler

Akizungumza baada ya Israel kupendekeza masharti yake yenyewe kwa ajili ya makubaliano hayo, Rais Obama amekiambia kituo cha redio cha NPR nchini Marekani kwamba masharti ya kuitaka Iran kuitambua Israel yanakwenda mbali kabisa na makubaliano.

"Dhana kwamba tungelipaswa kuiwekea masharti Iran ya kutokuwa na silaha za nyuklia kwa kuitambua kwake Israel ni sawa na kusema kwamba hatutasaini makubaliano mpaka utawala mzima wa Iran ubadilike moja kwa moja, na nadhani huko ni kupotosha," alisema Obama.

Serikali ya Israel - taifa pekee linalomiliki silaha za kinyuklia kwenye eneo zima la Mashariki ya Kati na Ghuba - ilikasirishwa sana na makubaliano ya awali yaliyotangazwa wiki iliyopita, baada ya mazungumzo ya muda mrefu kati ya Iran na mataifa makubwa duniani, na ambayo yanatazamiwa kukamilishwa kufikia tarehe 30 Juni mwaka huu.

Israel inadai makubaliano hayo ni mabaya kwa kila mtu na tayari imejitangazia haki ya kutumia nguvu ikiwa njia za kidiplomasia kuizuia Iran isiwe na silaha za nyuklia zitashindwa.

Netanyahu aja na masharti yake

Juzi Jumapili (Aprili 5), Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alitaka sharti la Iran kutambua haki ya kuwepo kwa taifa lake la Kiyahudi liwekwe kwenye makubaliano hayo, huku waziri wake wa usalama, Yuval Steinitz, akisema ahadi ya Obama kuendelea kuisadia Israel kulinda usalama wake haiondoshi kitisho kilichopo ikiwa Iran itamiliki silaha za nyuklia.

"Ikiwa Iran ina silaha za nyuklia, itakuwa kitisho kwa uwepo wa Israel. Hakuna anayeweza kutuambia kuwa kutusaidia na kutuunga mkono kunatosha kukizuia kabisa au kukilainisha kitisho hicho," alisema Steinitz mbele ya waandishi wa habari, huku akipendekeza makubaliano hayo yaweke kipengele cha kuizuia kabisa Iran kufanya utafiti na hata kufungwa moja kwa moja kwa kiwanda ya Fordo kinachorutubisha madini ya uranium.

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.Picha: picture-alliance/dpa/EPA/D. Hill

Serikali ya Rais Obama inajitayarisha kuyawasilisha na kuyatetea makubaliano hayo kwenye bunge linalotawaliwa na chama cha Republican chenye msimamo mkali unaoelemea Israel. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Marekani na Umoja wa Ulaya zitaondosha vikwazo vyao dhidi ya Iran, huku nayo Iran ikipunguza asilimia 98 ya kiwango chake cha madini ya uranium yaliyorutubishwa kwa kipindi cha miaka 15, na pia kuzuia kinu chake cha Arak kuzalisha madini ya plutonium yanayoweza kutengeneza silaha.

Siku ya Jumatatu (Aprili 6) Rais Obama alizungumza kwa njia ya simu na Mfalme Qaboos wa Oman juu ya yale yaliyomo kwenye makubaliano hayo. Obama alimueleza Qaboos kwamba muda uliopo kutoka sasa hadi Juni, utatumika kukamilisha masuala ya kiufundi ili kuhakikisha kuwa Iran inasalia na programu ya kinyuklia iliyo salama.

Obama amewaalika viongozi kadhaa wa mataifa ya Ghuba kujadiliana naye wasiwasi wao juu ya makubaliano hayo, ikiwemo Saudi Arabia - hasimu mwengine mkubwa wa Iran.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Hamidou Oummilkheir