1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama akubali uteuzi wa chama cha Democratic

7 Septemba 2012

Rais wa Marekani Barack Obama amekubali uteuzi wa chama chake, Democratic, kugombea muhula wa pili wa Urais. Katika hotuba yake Obama amesema itachukua muda kupata suluhisho kwa changamoto zinazoikabili nchi yao.

https://p.dw.com/p/164nJ
Rais Baraka Obama akukubali uteuzi wa chama cha Democratic
Rais Baraka Obama akukubali uteuzi wa chama cha DemocraticPicha: reuters

 Ilikuwa wakati wa hotuba yake kwenye kilele cha mkutano mkuu wa chama hicho, ambao umefanyika katika mji wa Charlotte, katika jimbo la North Caroline.

Akizungumza mbele ya wajumbe 6000 katika mkutano huo, Obama amesema katika uchaguzi wa mwezi Novemba ambamo atakuwa akipambana na Mitt Romney wa chama cha Republican, wamarekani watakuwa wakichagua juu ya mielekeo miwili tofauti kwa Marekani.

Njia ndefu kuukarabati uchumi

Mkutano mkuu wa Chama cha Democratic uliomalizika mjini Charlotte, North Carolina
Mkutano mkuu wa Chama cha Democratic uliomalizika mjini Charlotte, North CarolinaPicha: Reuters

Amekiri kwamba nchi inakabiliwa na changamoto kiuchumi, lakini akasema changamoto hizo zinaweza kupatiwa ufumbuzi.

''Itachukua miaka michache mingine kuweza kuukwamua uchumi ambao umekuwa ukiporomoka kwa miongo kadhaa. Itahitaji juhudi za pamoja, kuwajibika kwa kila mmoja wetu, na ujasiri kama ule wa Rais Franklin Roosevelt wakati wa mgogoro mkubwa pekee kuliko huu wa sasa''. Amesema Obama.

Rais Barack Obama alimshambulia mpinzani wake, Mitt Romney na chama cha Republican, akisema ni mtu asiyekuwa na uzoefu na ambaye hajali. Amemshutumu kutaka kuwapunguzia kodi matajiri wenzake na kuwatelekeza wamarekani wa tabaka la kati. Amesema Mitt Romney bado amefunikwa na wingu la enzi za vita baridi, kwa kuichukulia Urusi kuwa adui nambao moja wa Marekani, badala ya Al-Qaida.

Mivutano na papara

Rais Obama amemshutumu mpinzani wake, Mitt Romney, kutaka kuchochea mivutano
Rais Obama amemshutumu mpinzani wake, Mitt Romney, kutaka kuchochea mivutanoPicha: rtr

Ama kuhusu masuala ya usalama, Obama amesema wapinzani wake wa Republican wanaazimia kuirudisha nchi kwenye hali ya mivutano na kuchukua maamuzi ya kupapukia. Amesema sera yake ni kupunguza vita na kutumia fedha zitakazookolewa kuukarabati uchumi.

Wazungumzaji wakuu katika siku ya mwisho ya mkutano mkuu wa chama cha Democratic,wakiwemo John Kerry aliyewahi kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho, Makamu wa rais Joe Biden na Rais Barack Obana mwenyewe, wametilia msisitizo kuuawa kwa kiongozi wa Al-Qaida Osama bin Laden kama hatua muhimu katika juhudi ya kuimarisha usalama wa Marekani.

Suala jingine lililopewa kipaumbele katika hotuba ya viongozi wa chama cha Democrats ni mpango wa bima ya Afya wa Obama, ambao unapingwa vikali na chama cha Republican.

Obama, Romney, sambamba katika kura za maoni

Wademocrats wanasema mkutano wao mkuu ulikuwa wa mafanikio
Wademocrats wanasema mkutano wao mkuu ulikuwa wa mafanikioPicha: Reuters

Ikiwa inasalia miezi miwili tu hadi uchaguzi wa mwezi Novemba, Rais Obama na mpinzani wake Mitt Romney bado wako sambamba katika kura za maoni, wademocrats wanazinadi sera zao kuhusu masuala ya usalama, haki za wanawake na mashoga, uokozi wa sekta ya viwanda vya magari na kuuawa kwa Osama bin Laden kujaribu kumpa msukumo Rais Obama aweze kumpita mpinzani wake.

Barack Obama ambaye kampeni yake inamuonyesha kama mtu anayejali zaidi wamarekani wa kawaida na haki ya kila raia kutimiza ndoto yake, amehitimisha hotuba yake kwa kuwataka watu wenye maoni kama yake kumuunga mkono.

Amesema, ''Kama una imani katika nchi ambayo inampa haki kila raia, na ambako watu wote wako sawa mbele ya sheria, basi, naomba kura yako katika uchaguzi wa mwezi Novemba''.

Maafisa wa chama cha Democrats wameuchukulia mkutano wao mkuu kuwa wa mafanikio makubwa, na ambao umeweza kuamsha hamasa ya wapiga kura.

Mwandishi: Daniel Gakuba/RTRE/dpae/AFPE

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman