1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama akutana na viongozi wa nchi za Ghuba

Admin.WagnerD14 Mei 2015

Rais wa Marekani Barack Obama anakutana leo (14.05.2015) na viongozi wa nchi za Ghuba katika eneo lake la mapumziko la Camp David, akiwa na matumaini ya kuukoa mkutano wa kilele ulionuiwa kuondosha tofauti zilizopo.

https://p.dw.com/p/1FPiD
US-Präsident Obama trifft Anführer der Golfstaaten in Washington
Picha: AFP/Getty Images/N. Kamm

Eneo la mapumziko la rais wa Marekani, Camp David, ambalo linahusishwa na mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati wakati utawala wa rais wa zamani wa nchi hiyo Jimmy Carter na Bill Clinton, kwa mara nyingine tena litakuwa eneo la juhudi za maridhiano.

Rais Obama anakabiliwa na kibarua kigumu cha kuwashawishi wafalme, wana wa wafalme na mashehe wa eneo la Ghuba kwamba msimamo wake wa kuwa tayari kufanya mazungumzo na Iran kuhusu mpango wake wa nyuklia wenye utata, hauna maana anawaacha washirika wake wa muda mrefu.

Obama anatarajiwa kuwahakikishia usalama na kuwaahidi msaada zaidi wa kijeshi, yakiwemo mazoezi ya pamoja ya kijeshi na ushirikiano zaidi katika mifumo ya ulinzi dhidi ya makombora.

Kabla ya mkutano wa leo rais Obama jana alikutana na wana wa mfalme kutoka Saudi Arabia katika ikulu yake mjini Washington ambapo alisifu uhusiano na ushirikiano maalumu kati ya Marekani na Saudi Arabia ulioanza enzi za utawala wa raia wa zamani, Franklin Roosevelt na Mfalme wa zamani wa Saudi Arabia, Mfalme Faisal, katika miaka ya 1940.

Obama aliwapongeza mwanamfalme Mohammed bin Nayef na naibu mwanamfalme anayetarajiwa kurithi ufalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman, kwa kazi yao katika kupambana na ugaidi, ambayo aliileza kuwa ya umuhimu mkubwa kwa Marekani.

"Ufalme wa Saudi Arabia ni kiungo muhimu katika muungano wetu unaopambana dhidi ya kundi la dola la kiislamu na nina hakika tutakuwa na fursa ya kuujadili pia ufanisi uliopatikana katika vita dhidi ya kundi hilo nchini Iraq pamoja na mzozo unaoendelea nchini Syria."

Suala la Iran laibua mvutano

Lakini katika hatua ya kushangaza, Mfalme Salman wa Saudi Arabia hakuwepo katika kikao kilichofanyika ikulu, baada ya kukataa kuhudhuria kwa kile kinachoonekana kuwa mvutano wa kidiplomasia, licha ya serikali ya mjini Riyadh kukanusha.

US-Präsident Obama trifft Anführer der Golfstaaten in Washington Mohammed bin Nayef Saudi Arabien
Rais Obama (kulia) na Mwanamfalme Mohammed bin Nayef SaudiPicha: Reuters/K. Lamarque

Viongozi wengine watano wa eneo la Ghuba, wakiwemo wawili wa nchi kutoka Qatar na Kuwaiti, waliwasili baadaye katika ikulu ya Washington kwa kikao cha faragha na wanakwenda pia Camp David. Kauli ya Obama ilificha hali ya kutoelewana kuhusu suala la Iran, katika uhusiano ambao tayari umevurugwa na hatua yake ya kuyakumbatia kwa haraka mapinduzi ya msimu wa machipuko katika mataifa ya kiarabu na kupunguza hali ya kuyategemea mafuta kutoka eneo la Ghuba.

Akizungumzia uhusiano kati ya Marekani na Saudi Arabia, Mwanamfalme Mohammed bin Nayef, alisema, "Tunatafuta kuimarisha na kuutanua uhusiano wetu wa kihistoria kadri wakati unavyokwenda. Tunatarajia kushirikiana kwa karibu na kufanya kazi pamoja nawe kuzishinda changamoto zinazolikabili eneo letu na kurejesha hali ya utulivu na uthabiti."

Mataifa ya Ghuba yatatafuta kupata uhakika kutoka wa rais Obama kwamba yuko tayari kukabiliana na makundi yanayoisaidia Iran hususan nchini Syria ambako amekuwa akisitisita kuchukua hatua, hata kama kutasababisha changamoto kwa mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran. Viongozi watataka pia kuhakikishiwa kwamba mkataba wa nyuklia na Iran haumaanishi kutakuwa na mazungumzo mapana zaidi na Iran.

Mwandishi:Josephat Charo/AFP/APE

Mhariri:Daniel Gakuba