1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama akutana na wanahabari kwa mara ya mwisho

Grace Kabogo
19 Januari 2017

Rais wa Marekani, Barack Obama amekutana kwa mara ya mwisho na waandishi wa habari katika Ikulu ya Marekani, White House ambapo pamoja na mambo mengine amezungumzia mvutano kati ya Israel na Palestina na uhuru wa habari.

https://p.dw.com/p/2W22X
USA - Barack Obama hält letzte Rede als Präsident
Picha: Getty Images/AFP/N. Kamm

Katika tukio hilo la mwisho kwa Rais Obama kabla ya rais mteule Donald Trump kuchukua madaraka hapo kesho, katika masuala ya kimataifa, kiongozi huyo amekiri kwamba ana wasiwasi kuhusu suluhisho la mataifa mawili kutokana na mzozo unaoendelea kati ya Israel na Palestina, ikiwemo ujenzi wa makaazi ya Walowezi katika Ukingo wa Magharibi.

''Nina wasiwasi kuhusu pande zote mbili kwa sababu nadhani hali iliyopo ni endelevu. Hali ni hatari kwa Israel, suala hilo ni hatari kwa Wapalestina, hali ni mbaya katika ukanda wa Mashariki ya Kati na pia ni hatari kwa usalama wa taifa la Marekani,'' alisema Obama

USA Mittlerer Osten Friedensgespräche Benjamin Netanyahu und Mahmoud Abbas
Kiongozi wa Palestina, Mahmoud Abbas (Kushoto) na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu (Kulia)Picha: picture-alliance/dpa

Rais Obama amesema serikali yake haikulizuia azimio la hivi karibuni la Umoja wa Mataifa kuhusu shughuli za ujenzi wa makazi ya Walowezi katika ardhi ya Wapalestina inayokaliwa na Israel, kwa sababu iliona kwamba suluhisho la mataifa mawili ndiyo njia bora ya kupatikana kwa amani.

Amebainisha kuwa hataki kutabiri kile kinachoweza kutokea, akimaanisha dhahiri mpango wa Trump wa kutaka kuuhamisha ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv kwenda Jerusalem. Amemuonya Trump dhidi ya kuchukua hatua za upande mmoja kuhusu mji wa Jerusalem.

Uhuru wa vyombo vya habari

Obama pia amezungumzia kuhusu uhuru wa vyombo vya habari na kusema kwamba demokrasia haiwezi kufanikiwa vizuri, kama hakuna raia ambao wamepata habari vizuri na kulikuwa na kazi muhimu ya kuanzisha misingi ya ukweli na ushahidi. Amebainisha kuwa uhuru wa habari ni sehemu ya jinsi Marekani inavyofanya kazi kama taifa.

Ama kwa upande mwingine Rais Obama ametetea maamuzi yake ya mwisho aliyochukua akiwa madarakani, ukiwemo uamuzi wa kupunguza kifungo cha miaka 35 jela dhidi ya Chelsea Manning, aliyevujisha maelfu ya nyaraka za siri kwa mtandao wa kufichua siri wa Wikileaks. Amesema Manning alifikishwa mahakamani na kujutia makosa yake aliyoyafanya mwaka 2010.

USA Chelsea Manning Transgender Soldat
Chelsea Manning Picha: picture-alliance/AP Photo/U.S. Army

Amesema Manning aliyekuwa mchambuzi wa masuala ya kijasusi wa jeshi, ametumikia vizuri kifungo chake gerezani na atatumika kama njia ya kuzuia mtu yeyote kufikiria kufanya kitendo kama hicho. Obama amesema ameridhika kwamba haki imefanya kazi vizuri.

Rais Obama pia amezungumzia maisha yake baada ya kuondoka madarakani, akisema atatumia muda mwingi kwa ajili yake mwenyewe pamoja na familia yake. Obama pia amethibitisha kuwa atahudhuria sherehe za kuapishwa Trump, tofauti na ilivyo kwa baadhi ya wanachama wenzake wa Democratic.

Mkutano wa jana na waandishi wa habari ulikuwa wa 39 akiwa mwenyewe, wa 21 akiwa katika chumba cha mikutano cha habari cha Ikulu ya White House na wa 224 kwa ujumla wa mikutano yote ya waandishi wa habari.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/Reuters, DW, AFP
Mhariri: Idd Ssessanga