1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama alaani mauaji ya Misri

Admin.WagnerD15 Agosti 2013

Rais Barack Obama wa Marekani amesema Misri imeingia katika njia ya hatari, na kutangaza kuwa nchi yake imefuta mazoezi ya pamoja ya kijeshi na nchi hiyo kupinga mauaji dhidi ya raia.

https://p.dw.com/p/19QcM
Watu zaidi ya 500 waliuawa katika ghasia za Jumatano mjini Cairo
Watu zaidi ya 500 waliuawa katika ghasia za Jumatano mjini CairoPicha: Reuters

Kauli ya rais Obama ambayo ni ya kwanza tangu mauaji ya jana mjini Cairo, ameitoa akiwa likizoni katika jimbo la Massachussetts. Barack Obama amesema amechukizwa na jinsi serikali ya Misri ilivyowashughukia waandamanaji, na kuonya kuwa hatua mienendo ya serikali hiyo imeathiri uhusiano kati ya nchi hizo mbili.

''Uhusiano wetu wa kijadi hauwezi kuendelea kama kawaida, huku raia wakiwa wanauawa mitaani, na haki zao zikikanyagwa''. Amesema rais Obama na kuongeza kuwa kutokana na hali hiyo, Marekani imeiarifu serikali ya Misri, kwamba mazoezi ya kijeshi ya pamoja yaliyokuwa yamepangwa mwezi ujao kati ya nchi hizo yamefutwa. ''Nimewaomba maafisa wangu wa usalama kutafakari athari za hatua zilizochukuliwa na serikali hiyo, na hatua ambazo tunaweza kuzichukua sisi, katika uhusiano wetu na Misri.'' Ameendelea kusema rais Barack Obama.

Rais Obama amesema uhusiano na Misri hauwezi kuendelea kama kawaida
Rais Obama amesema uhusiano na Misri hauwezi kuendelea kama kawaidaPicha: Reuters

Ofisi za serikali zachomwa moto

Wakati hayo yakijiri, taarifa za vyombo vya habari nchini Misri zimeeleza kuwa kundi la wafuasi wa udugu wa kiislamu lililojawa na ghadhabu, limeyachoma moto majengo mawili ya serikali katika mji wa Giza ulio karibu na Cairo, katika eneo ambalo ni maarufu kwa mapiramidi. Mwandishi wa shirika la habari la Associated Press amesema kuwa ameshuhudia majengo hayo yakiwaka moto. Picha za televisheni zimeonyesha wazima moto wakiwasaidia wafanyakazi kutoka ndani ya jengo mojawapo.

Habari zaidi zimeeleza kuwa wafuasi hao wa udugu wa kiislamu vile vile wamevishambulia vituo vya polisi katika eneo la Sinai na katika mji wa Assiut ulio katikati mwa nchi, na kuwauwa maafisa wawili wa usalama katika mashambulizi hayo.

Hali hii ya kuenea kwa wasiwasi inafuatia operesheni kubwa iliyoendeshwa na jeshi dhidi ya waandamanaji wanaomuunga mkono rais aliyepinduliwa Mohamed Mursi, ambao kwa takribani wiki sita walikita kambi katika maeneo mawili ya mji mkuu Misri, wakishinikiza Mursi arejeshwe madarakani. Takwimu rasmi za serikali zimesema watu 525 waliuawa katika operesheni hiyo.

Ofisi ya serikali iliyochomwa moto na wafuasi wa Mursi
Ofisi ya serikali iliyochomwa moto na wafuasi wa MursiPicha: Reuters

Dunia yaungana kupinga mauaji ya raia

Viongozi wa mataifa mbali mbali duniani wameendelea kuelezea kuchukizwa kwao na mauaji hayo. Marekani ilisema mauaji hayo ni ya kulaaniwa vikali, na mabalozi wa Misri nchini Ufaransa, Uingereza, Ujerumani na Italia, waliitwa na serikali za nchi hizo, na kujulishwa rasmi kuwa nchi hizo zimechukizwa na ghasia hizo.

Waziri Mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amekwenda mbali zaidi na kutaka kiitishwe kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kujadili kile alichokiita mauaji ya halaiki yaliyofanywa dhidi ya waandamanaji.

Kiongozi wa kanisa katoliki ulimwenguni Papa Francis amesema anawaombea wahanga wa ghasia zinazoendelea nchini Misri, na kutoa wito wa kuwepo kwa amani, mjadala na maridhiano.

Na mkuu wa kitengo cha Umoja wa Mataifa cha Haski za binadamu Navi Pillay, ametoa wito wa kufanyika uchunguzi wa kina, juu ya namna vyombo vya usalama vya Misri vilivyowashughulikia wandamanaji, na kusababisha umwagikaji mkubwa wa damu.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFP/AP

Mhariri: Josephat Charo