1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama amuidhinisha Hillary Clinton kuwa mrithi wake

Yusra Buwayhid10 Juni 2016

Rais wa Marekani Barack Obama ametangaza kumuunga mkono Hillary Clinton kuwa mgombea urais wa chama cha Democratic, katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Novemba mwaka huu nchini Marekani.

https://p.dw.com/p/1J4Df
USA Präsidentschaftswahlkampf Barack Obama unterstützt Clinton
Picha: picture-alliance/dpa/R. Sachs

Obama alimuidhinisha aliyekuwa waziri wake wa mambo ya nje Hillary Clinton kuwa ndiye mrithi wake hapo jana, na amewasisitiza wafuasi wote wa chama cha Democratic kufanya hivyo.

"Naujua ugumu wa kazi hii. Na ndiyo maana najua kwamba Hillary ataifanya vizuri hii kazi. Kwa kweli, sidhani kama kumewahi kutokea mtu aliye na uwezo kama wake wa kupokea wadhifa huu. Ni mtu mwenye ujasiri, huruma, na moyo wa kufanya kazi," amesema Obama kupitia mkanda wa video wa mtandaoni.

Clinto amesema amefurahishwa sana kwa kuungwa mkono na Obama, katika kampeni yake ya kuelekea uchaguzi wa Novemba 8.

Mwingine kutoka chama cha Democratic aliyemuunga mkono Clinton, ni Seneta wa jimbo la Massachusetts Elizabeth Warren, ambaye vyombo vya habari nchini humo vinasema huenda akawa mgombea mweza wa Clinton.

USA Präsidentschaftswahlkampf Senatorin Elizabeth Warren
Elizabeth warren, Seneta wa jimbo la Massachusetts MarekaniPicha: picture-alliance/AP Photo/N. Wass

“Niko tayari, niko tayari kuungana na Hillary Clinton katika vita hivi mpaka awe rais wa Marekani, kufanya naye kazi kwa moyo wangu wote na kuhakikisha Donald Trump kamwe hapati nafasi hata kidogo ya kuingia Ikulu ya Marekani," amesema Warren.

Clinton pia amesema anamuheshimu sana Warren, na yuko radhi kupokea mawazo yake mazuri na msaada wake.

Makamu wa Rais Joe Biden, pia ni miongoni mwa viongozi wa Democratic waliomuunga mkono Clinton. Katika hotuba yake mjini Washington Biden amesema, "yoyote yule atakayekuwa rais ajaye, lakini Mungu akipenda atakuwa Clinton."

Obama amtaka Sanders ajitoe katika kampeni

Uungwaji mkono huwo unakuja baada ya Obama kukutana na Bernie Sanders, ambaye ni mgombea mwengine wa chama hicho na kumtaka ajitoe katika kampeni. Na badala yake amuunge mkono Clinton, ili kwa pamoja waweze kumshinda Donald Trump wa chama cha Republican.

Obama na viongozi wengine wa chama cha Democratic wanajaribu kumtafutia uungwaji mkono mkubwa Clinton ndani ya chama hicho, lakini bila ya kumtenga Sanders na wafuasi wake.

Katika kile kinachoonekana kama kujaribu kumshawishi Sanders kuachana na kampeni yake ya kugombea urais, Obama alikutana naye Ikulu ya Marekani mjini Washington hapo jana.

Na baada ya mkutano huwo, Sanders aliwaambia wanahabari bado ataendelea kupambana hadi mwisho. Ambayo ni siku ya mkutano mkuu wa chama, Ijumanne ijayo. Lakini pia Sanders amesema atafanya kazi pamoja na Clinton, kumshinda Donald Trump.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/rtre/ape/

Mhariri: Mohammedn Khelef