1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama ana kipaji cha kuona mambo kama yalivyo

P.Martin - (DPAE)9 Machi 2009

Mzozo wa kampuni la magari Opel na lawama kuwa Kansela Merkel hana msimamo bayana wakati uchaguzi mkuu ukikaribia ni miongoni mwa mada zilizogonga vichwa vya habari katika magazeti ya Ujerumani leo siku ya Jumatatu.

https://p.dw.com/p/H8PK

Lakini tutaanza na habari inayohusika na uwezekano kwa Marekani kuzungumza na Wataliban wenye msimamo wa wastani. Gazeti la BADISCHE NEUESTE NACHRICHTEN linasema:

"Rais wa Marekani Barack Obama ana kipaji cha kuweza kuona mambo vile yalivyo.Yeye anaelewa vizuri kipi kinachomngojea huko Afghanistan. Vietnam ya pili-yaani vita virefu visivyoungwa mkono na ukiwepo pia uwezekano wa kuishia vibaya.Akitambua ukweli huo,ndio anazingatia kuwatenganisha Wataliban kwa kujaribu kuzungumza na wale wasio na misimamo mikali.Labda hiyo ndio njia pekee ya kufanikiwa."

Gazeti la LEIPZIGER VOLKSZEITUNG likiandika kuhusu hali ya kutoridhika na ukosefu wa msimamo bayana wa Kansela wa Ujerumani Angela Merkel linasema:

"Merkel yupo hatarini kuitumia vibaya nafasi yake kwani wapiga kura wanaounga mkono chama chake cha CDU wanakosa kuelezwa waziwazi msimamo wa kiongozi huyo.Hapo kuna hatari ya wanachama hao kukimbilia chama cha kiliberali cha FDP au kuamua kususia kabisa uchaguzi ujao. Merkel anapaswa kufahamu kuwa iwapo atawakorofisha wapiga kura wa CDU na hata FDP basi uwezekano wa kubakia Kansela baada ya uchaguzi,utafifia."

Mada nyingine inayoendelea kuchomoza katika magazeti ya Ujerumani ni mzozo wa kampuni la magari Opel linalokabiliwa na matatizo ya fedha.Gazeti la SÄCHSISCHE ZEITUNG linaeleza hivi:

"Ukweli kuwa kampuni la Opel lilikuwa likilipa kodi yake nchini Marekani badala ya huku Ujerumani isiwe sababu ya kutovisaidia viwanda vya Opel na kuviepusha kwenda muflisi hata ikiwa ukweli uliojulikana unahamakisha. Kwani mtindo wa kulipa kodi katika nchi nyingine si marufuku - sheria za Ujerumani zinaruhusu kufanya hivyo.Hata makampuni ya Kijerumani yaliyo na viwanda nchi za nje hayalipi kodi kwa faida zinazopatikana huko.Mtindo huo hauvutii,lakini hiyo isiwe sababu ya kuwaadhibu waajiriwa wa Opel."

Tunamalizia kwa mkasa wa majengo yaliyoporomoka mjini Cologne juma lililopita. Gazeti la KÖLNISCHE RUNDSCSHAU linasema:

"Mkuu wa shirika la usafiri mjini Cologne KVB amechukua muda mrefu kujieleza.Jürgen Fenske ameomba msamaha siku sita baada ya kuporomoka kwa jengo lililokuwa likihifadhi hati muhimu za kihistoria. Hatimae shirika la KVB limetambua kuwa mbali na kuwajibika kisheria kama wajenzi wa njia inayochimbwa chini kwa chini katika eneo hilo, wakuu wa shirika hilo wanapaswa pia kujibu masuala yanayozuka badala ya kubakia kimya. Lakini kueleza kuwa kuna hatari kokote kule kunapojengwa,haisaidii kabisa kuleta imani."