1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama ana matumaini na mazungumzo ya Iran

Mohammed Khelef20 Machi 2015

Rais Barack Obama wa Marekani anasema kuna uwezekano mwaka huu ukaleta mafanikio kwenye mahusiano kati ya nchi yake na Iran kupitia mazungumzo juu ya mpango wa nyuklia wa Iran yanayokwenda vyema.

https://p.dw.com/p/1EuNx
Rais Barack Obama wa Marekani.
Rais Barack Obama wa Marekani.Picha: Reuters/Jonathan Ernst

Katika kile kilichopewa jina la "ujumbe wa Rais Obama kwa watu na viongozi wa Iran" kuadhimisha mwaka mpya wa Nowruz wa Kiirani, kiongozi huyo wa Marekani amesema anaamini mataifa hayo mawili yana nafasi ya kihistoria kuumaliza mzozo wa nyuklia na kwamba hayapaswi kuiwacha fursa hiyo ikapotea.

"Ujumbe wangu kwenu watu wa Iran ni kwamba kwa pamoja tunapaswa kuzungumzia mustakabali tunaoutafuta. Kama ambavyo nimeshasema mara kadhaa, ninaamini nchi zetu lazima ziweze kulimaliza suala hili kwa amani, kwa diplomasia," alisema Obama kwenye ujumbe huo.

Rais Obama alisema ni jambo la kutia moyo kwamba "kiongozi mkuu wa Iran, Ayatullah Khamenei, ametoa fatwa dhidi ya uundwaji wa silaha za nyuklia, na Rais Rouhani amesema Iran kamwe haitatengeneza silaha hizo," akiongeza kwamba kwa kushirikiana na jumuiya ya kimataifa "Marekani imesema kwamba Iran inastahiki kuwa na nishati ya nyuklia kwa matumizi ya amani, kulingana na wajibu wa Iran kimataifa."

Iran na mataifa sita yenye nguvu duniani yanajaribu kufikia makubaliano ya kuudhibiti mpango huo ya nyuklia kwa kipindi cha angalau miaka 10 ili nayo Iran iondolewe vikwazo hatua kwa hatua.

Mataifa hayo yanakusudia kukamilisha utaratibu wa makubaliano hayo kufikia mwishoni mwa mwezi huu wa Machi, na ambapo mkataba rasmi unatazamiwa kupatikana tarehe 30 Juni.

Bado hakujapatikana muafaka

Mjini Brussels, mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya, Federica Mogherini, atafanya mazungumzo na viongozi wa Uingereza, Ufaransa na Ujerumani hivi leo juu ya programu hiyo ya nyuklia ya Iran.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif (kulia), na mwenzake wa Marekani, John Kerry.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif (kulia), na mwenzake wa Marekani, John Kerry.Picha: Reuters/Brian Snyder

Mkutano wa viongozi hao wanne, unafanyika wakati Iran ikiendelea na mazungumzo nchini Uswisi, ambako Waziri wake wa mambo ya nje, Mohammad Javad Zarif anakutana na mwenzake wa Marekani, John Kerry.

Wote wawili wamesema kuwa hatua kubwa imepigwa kwenye mazungumzo yao, ingawa afisa mmoja wa Umoja wa Ulaya kwenye mazungumzo hayo amesema bado pande hizo hazina dalili ya kuafikiana.

Katika hotuba yake ya hapo jana usiku kwa watu wa Iran, Rais Obama alisema kwamba wiki zinazofuatia kuanzia sasa zitakuwa muhimu sana kwa pande zote zinazoshiriki kwenye mazungumzo hayo, kwani ndizo zitakazofungua milango iliyokuwa imefungwa muda mrefu kati ya Iran na ulimwengu, hasa kwenye biashara, uwekezaji, elimu na sayansi.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Saumu Yusuf