1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama ashinda katika jimbo la Mississippi

Mwakideu, Alex12 Machi 2008

Seneta wa Ilinois Barack Obama amemshinda mpinzani wake Hillary Clinton huku siasa za ubaguzi wa rangi zikiibuka

https://p.dw.com/p/DNBO
Wawaniaji wa kiti cha Urais kwa tikiti ya chama cha Demokratik; Hillary Clinton na Barrack ObamaPicha: AP

Seneta wa Ilinois Barack Obama amemshinda mpinzani wake Hillary Clinton katika uteuzi wa kuwania tiketi ya chama cha Demokrat uliofanyika Mississippi.


Ushindi wa Obama umetokea wakati ambapo kumezuka mjadala mkali kuhusu ubaguzi wa rangi katika kampeni zao za kuwania kiti cha Urais.


Seneta wa jimbo la Illinois Barrack Obama amerejelea ushindi wake wa kufululiza kwa kushinda mara mbili mfululizo baada ya Hillary Clinton mkewe Rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton kumshinda katika maeneo ya Texas na Ohio wiki jana. Ushindi wa Clinton ulikuja baada Obama kumshinda mara 12 mfululizo.


Lakini licha ya kusherehekea ushindi wa Mississipi kambi ya Obama imetoa wito wa kuondolewa kwa mfuasi wa Clinton Geraldine Ferraro katika kampeni hizo kufuatia matamshi ya bwana huyo kwamba ushindi wa Obama unatokana na rangi yake.


Feraro aliambia gazeti moja la California kwamba iwapo Obama angekuwa mtu mweupe basi hangetamba katika kampeni zake.


Obama aliyataja matamshi hayo ya mwanamke aliyepigania kiti cha makamu wa Rais kwa tikiti ya chama cha demokrat mwaka wa 1984 kama ya kipuuzi.


Jimbo la Mississipi lenye wajumbe 33 na ambalo linaaminika kuwa na wafuasi wengi wa chama cha republican ndio eneo muhimu la mwisho katika uteuzi wa chama cha demokrat kabla ya ule wa Pennsylvania utakaofanyika aprili 22.


Akiongoe na wanahabari baada ya ushindi wake Obama alielezea furaha zake akisema kwamba ushindi huo katika maeneo ya Wycoming na Mississippi umemmuongezea wajumbe na kwamba wanachokifanya ni kuhakikisha habari za mabadiliko wanazieneza katika kila pembe za nchi ya Marekani.


Katika taarifa yake Obama amesema watu wa Mississippi wameungana na mamilioni ya wamarekani kutoka kila pembe za nchi hiyo ambao wameamua kubadili siasa za zamani zilizogonga mwamba na kukumbatia azimio lao la mabadiliko.


Jimbo la Mississippi halijabadilisha sana kinyanganyiro cha kuwania tikiti ya chama cha demokrat kati ya Obama na Hillary Clinton isipokuwa limemuongezea Obama wajumbe watakaoshiriki katika uteuzi wa mwisho wa kumpasisha mgombea wa kiti cha Urais kwa tikiti ya chama cha demokrat.


Msimamizi mkuu wa kampeni za Clinton, Maggie Williams amempongeza Obama kwa ushindi wake na kueleza kwamba wanaangalia mbele katika jimbo la Pennsylvania. Hata hivyo Clinton hajasikika akitoa pongezi zake kwa ushindi huo.


Baada ya asilimia 99 ya kura kuhesabiwa katika jimbo la Mississippi Obama ameshinda kwa asilimia 61 ya kura ikilinganishwa na asilimia 37 alizopata Clinton.


Nusu ya wapiga kura walioshiriki katika uteuzi huo wa chama cha democrat walikuwa waafrika wamarekani. Kura tisa kati ya kumi walizopiga zilimuendea Obama.


Asilimia 69 hadi 30 ya kura za waume wazungu zilimuendea Clinton huku wake wazungu wakimpatia asilimia 74 hadi 26 ya kura zao.


Kulingana na hesabu za RealClearPolitics.com ushindi wa Mississipi umempatia Obama wajumbe 1,606 ikilinganishwa na Clinton mwenye wajumbe 1,484. Wajumbe 2,025 ndio wanaohitajika kwa yeyote atakaeshikilia tikiti ya chama cha demokrat ili kupigania Urais nchini Marekani.