1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama ashutumu shambulio nchini Mali

21 Novemba 2015

Rais wa Marekani Barack Obama ameshutumu kile alichokiita, shambulio linalokera lililofanywa na wapiganaji wa jihadi nchini Mali ambapo watu 27 wameuwawa, ikiwa ni pamoja na raia wa Marekani.

https://p.dw.com/p/1H9tQ
Mali Geiselnahme Radisson Blu Hotel in Bamako
Hoteli ya Radisson Blu iliyovamiwa na magaidiPicha: picture-alliance/dpa

"Unyama huu unatuimarisha zaidi kupambana na changamoto hii," amesema Obama wakati akiwa ziarani nchini Malaysia, akidokeza kuhusu kitisho duniani kinacholetwa na matumizi ya nguvu ya makundi ya itikadi kali.

Wapiganaji wa jihadi wenye silaha waliwateka nyara zaidi ya watu 100 kwa zaidi ya masaa tisa katika hoteli katika mji mkuu wa mali Bamako siku ya Ijumaa(20.11.2015).

Mali Geiselnahme Hotel in Bamako Befreiung von Geiseln
Watu wakiokolewa kutoka katika hoteli ya Radisson Blu mjini BamakoPicha: Imago

Kundi la Al-Murabitoun lenye mahusiano na kundi la al-Qaeda likiongozwa na raia wa Algeria mwenye jicho moja Mokhtar Belmokhtar lilidai kuhusika na shambulio hilo.

Hofu imetanda

Tukio hilo limeongeza hofu kuhusiana na makundi ya jihadi duniani , wiki moja baada ya shambulio baya mjini Paris ambapo watu 130 waliuwawa na kundi la Dola la Kiislamu lilidai kuhusika na shambulio hilo.

Mali Geiselnahme Hotel in Bamako
Mwanamke akiokolewa na vikosi vya jeshiPicha: Imago

Vikosi maalum vilifanya msako ghorofa kwa ghrofa na kumaliza utekaji nyara huo baada ya masaa tisa. Vyanzo katika jeshi la usalama nchini Mali vimesema kiasi ya watu 27 waliotekwa nyara wameuwawa. Afisa mwandamizi wa wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani amethibitisha kwamba raia wa Marekani ni miongoni mwa wahanga ambapo Wamarekani wengine kadhaa wamenusurika katika shambulio hilo.

Wamarekani sita wamepatikana salama na vikosi maalum vya Marekani vilisaidia katika juhudi za uokozi, amesema afisa wa Marekani hapo kabla.

Mali Geiselnahme Hotel in Bamako
Mateka aliyejeruhiwa akipelekwa katika sehemu salamaPicha: picture-alliance/dpa

Mapema jana Ijumaa (20.11.2015)watu wenye silaha wakipiga kelele wakitamka kauli mbiu za Kiislamu walishambulia hoteli ya Radisson Blu, ambayo hutembelewa sana na wageni nchini humo, wakiwateka watu 170 mjini Bamako, mji mkuu wa Mali.

Kiasi ya watu 27 wanaripotiwa kuwa wameuwawa baada ya vikosi maalum vya jeshi la Mali kuvamia hoteli hiyo na watu kadhaa wanaripotiwa wamefanikiwa kuwatoroka watekaji nyara wao ama wameokolewa.

Wawakilishi wa kikosi cha jeshi la Marekani wamesema wanajeshi wa Marekani walisaidia kuwaweka raia katika usalama wakati majeshi ya Mali yakisafisha eneo la hoteli hiyo ya Radisson Blu.

Mali Geiselnahme Hotel in Bamako
Mateka wakisindikizwa na vikosi vya jeshi kwenda kwenye usalamaPicha: picture-alliance/dpa

Hali ya hatari yatangazwa

Rais Ibrahim Boubakar Keita ametangaza idadi ya watu waliofariki na kusema watu saba wamejeruhiwa katika shambulio hilo. rais Keita pia ametangaza hali ya hatari kwa muda wa siku 10.

Mali Geiselnahme Hotel in Bamako
Wanajeshi wakilinda doria karibu na hoteli ya Radisson Blu mjini BamakoPicha: H. Kouyate/AFP/Getty Images

Shambulio hilo ni pigo kubwa kwa mkoloni wa zamani wa taifa hilo Ufaransa ambayo imeweka wanajeshi 3,500 kaskazini ya Mali kujaribu kurejesha utulivu baada ya uasi mwaka 2012 uliofanywa na watu wa kabila la Tuareg ambao ulitekwa baadaye na wapiganaji wa jihadi wenye mahusiano na kundi la al-Qaeda.

Mwandishi : Sekione Kitojo / rtre

Mhariri: Isaac Gamba