1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama atangaza mpango wa dola bilioni 3 G20

Sekione Kitojo15 Novemba 2014

Rais Barack Obama leo (15.11.2014)ametangaza mchango wa Marekani wa dola bilioni 3 kwa mfuko wa kimataifa kuzisaidia nchi masikini duniani kupambana na athari za mabadiliko ya tabia nchi katika mkutano wa kundi la G20.

https://p.dw.com/p/1Dnvf
G 20 Gipfel in Brisbane 14.11.2014 B 20 Treffen
Viongozi wa G20 wakiwa mkutanoniPicha: Reuters/J. Reed

Leo natangaza kwamba Marekani itachukua hatua nyingine muhimu. Tutachangia dola bilioni 3 katika mfuko wa mazingira salama kuzisaidia nchi masikini kupambana na mabadiliko ya tabia nchi," amesema katika hotuba aliyoitoa katika chuo kikuu cha Queensland mjini Brisbane, ambako anahudhuria mkutano wa kundi la mataifa ya G20.

Wakati huo huo utaratibu wa aina ya enzi za vita baridi kati ya Urusi na mataifa ya magharibi umeleta hali ya wasi wasi katika mazungumzo ya kundi la mataifa ya G20 yanayokusudiwa kuchochea ukuaji wa uchumi wa dunia wakati viongozi hao wakianza mkutano wao mjini Brisbane nchini Australia.

Barack Obama ASEAN Gipfel in Myanmar 13.11.2014
Rais Barack Obama mjini BrisbanePicha: Reuters

Ongezeko la ujoto

Ongezeko la ujoto duniani ni suala lililojitokeza kupewa umbele na viongozi hao ikiwa ni pamoja na Barack Obama wa Marekani, Vladimir Putin wa Urusi na Xi Jinping wa China, na kusababisha hali ya mparaganyiko kwa wenyeji Australia baada ya nchi hiyo kulenga kuuelekeza mkutano huo katika masuala ya ukuaji wa uchumi wa dunia.

Waziri mkuu wa Australia Tony Abbott amewakumbusha wenzake wa G20 kwamba kwa pamoja nchi zao zinafanya jumla ya asilimia 85 ya pato jumla la taifa katika sayari hii yakiwa na asilimia 65 ya raia.

Dunia inapitia muda wa wasi wasi na inataka uhakika "kwamba kuna watu ambao wanafahamu kile wanachokifanya, kwamba kuna watu ambao wana mipango, mpango kwa ajili ya ukuaji na nafasi za ajira," amesema mwanzoni mwa mkutano huo.

Australien Wirtschaft G20-Gipfel in Brisbane David Cameron und Narendra Modi
David Cameron wa Uingereza katika mkutano wa G20Picha: Reuters/L. Koch

Abbott pia amewataka viongozi hao kutumia majina ya kwanza kutambuana , "kwasababu pamoja na tofauti zitakazokuwapo , nafikiri inasaidia iwapo kutakuwa na uhusiano mzuri wa binafsi miongoni mwetu."

Pamoja na hayo Abbott binafsi ameingia katika mkutano huo akipambana katika vita vya maneno na Vladimir Putin kuhusiana na kuangushwa kwa ndege ya abiria ya shirika la ndege la Malaysia katika anga ya Ukraine Julai mwaka huu.

Mapambano dhidi ya Ebola

Wakati huo huo Umoja wa Mataifa umewataka viongozi wa kundi la G20 kuongeza juhudi katika kupambana na ugonjwa hatari wa Ebola katika mataifa ya Afrika magharibi, ukionya kuhusu mzozo mkubwa wa chakual iwapo watashindwa kuchukua hatua.

Merkel Ankunft in Brisbane zu G 20 Gipfel 14.11.2014
Angela Merkel wa Ujerumani akiwasili katika mkutano wa G20Picha: Reuters/G20 Australia

Akizungumza mjini Brisbane ambako unafanyika mkutano wa G20 , katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amejiunga na mashirika ya kimataifa ya kutoa misaada kuwataka viongozi hao kuchukua hatua madhubuti kupambana na ugonjwa wa Ebola. Ban amesema wakati viwango vinapungua katika eneo moja, vinapanda katika upande mwingine.

Uambukizaji amesema unaendelea kuongezeka kuliko hatua zinazochukuliwa kupambana na ugonjwa huo kutoka jumuiya ya kimataifa.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre

Mhariri: Mohamed Dahman