1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama atoa hotuba ya mwisho kuhusu hali ya Taifa la Marekani

Caro Robi13 Januari 2016

Rais wa Marekani Barack Obama ametoa hotuba yake ya mwisho kuhusu hali ya taifa la Marekani. Amegusia masuala kadha wa kadha ikiwemo haja ya Wamarekani kuungana, uchumi na kitisho cha IS.

https://p.dw.com/p/1HcGB
Picha: picture-alliance/dpa/E. Vucci

Rais Obama amewataja wanamgambo wa kundi la Dola la Kiislamu IS kama wauaji wenye misimamo mikali ambao wanastahili kusakwa na kuangamizwa na kulitaka bunge la Marekani kuidhinisha matumizi ya nguvu za kijeshi kulikabili kundi hilo la IS akisema hata hivyo kwamba vita hivyo havitakuwa vita vya tatu vikuu vya dunia.

Obama amewataka Wamerakani ambao wanatiwa wasiwasi na kitisho cha ugaidi na hali ya kiuchumi kutohofu na badala yake wanahitaji kufanya maamuzi kati ya kuogopa mabadiliko au kuzikabili siku za usoni kwa ujasiri.

Katika matamshi yaliyoonekana kuwashutumu wagombea Urais wa chama cha Republican ambao wamekuwa wakiukosoa utawala wake kuhusu jinsi ilivyoshughulikia sera za kigeni na uchumi, Obama amesema Marekani imepitia nyakati ngumu katika kipindi cha nyuma na ni wakati wa kufanya mabadiliko ya kipekee ili kusonga mbele akiongeza kuwa madai kuwa uchumi unasusua ni uongo.

Ni wakati wa kukubali mabadiliko

Kiongozi huyo ambayehuu ni mwaka wake wa mwisho madarakani, amewataka wabunge wa taifa hilo kushughulikia masuala makubwa yanayoikabili nchi hiyo bila ya kuzingatia ni nani atakuwa Rais baada yake ikiwemo jinsi ya kutoa fursa za kiuchumi, kuimarisha teknolojia ili kuinua maisha ya watu, namna ya kuifanya Marekani kuwa salama na kuimarisha mazingira ya kisiasa nchini humo.

Rais wa Marekani Barack Obama akitoa hotuba yake ya mwisho mbele ya Bunge
Rais wa Marekani Barack Obama akitoa hotuba yake ya mwisho mbele ya BungePicha: Reuters/J.Bourg

Kuhusu sera yake ya kigeni Obama ameonekana kutetea mtizamo wake wa kutumia ushirikiano na washirika wengine kupitia juhudi za kidiplomasia badala ya kutumia zaidi nguvu za kijeshi.

Obama pia amesema Makamu wake Joe Biden ataongoza juhudi mpya za kuifanya Marekani kuwa taifa linaloweza kutibu kikamilifu saratani. Kiongozi huyo wa Marekani ambaye anamaliza muhula wake wa pili madarakani mwaka huu, pia amelitaka bunge kuliondolea vikwazo Cuba.

Obama asifu makubaliano ya kihistoria

Amepongeza kufikiwa kwa makubaliano ya kihistoria kama makubaliano ya mazingira ya Paris yanayolenga kupunguza joto duniani, makubaliano kati ya Iran na nchi zenye nguvu zaidi duniani kuhusu mpango wake wa kinyuklia na ufanisi katika kukabiliana na virusi vya Ebola katika nchi za magharibi mwa Afrika.

Mke wa Rais Obama Michelle Obama na Gavana wa Conneticut Dannel Malloy
Mke wa Rais Obama Michelle Obama na Gavana wa Conneticut Dannel MalloyPicha: picture-alliance/AP Photo/S.Walsh

Masuala mengine ambayo ameyaangazia katika hotuba yake ya mwisho ni kufungwa kwa gereza la Guantanamo ambapo amesema atajaribu kulifunga, kushughulikia mizozo duniani hasa katika kanda ya mashariki ya kati, mabadiliko ya hali ya hewa, nishati na vita dhidi ya Malaria.

Rais huyo amekiri kuwa wakati wa utawala wake mvutano baina ya vyama vikuu nchini Marekani ulishamiri badala ya kupungua, akisema hali hiyo ni mojawapo ya masuala machache anayojutia katika kipindi chake kama Rais.

Mwandishi: Caro Robi/afp/reuters/dpa

Mhariri: Gakuba Daniel