1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama awasili nchini Ethiopia

26 Julai 2015

Rais Barack Obama amewasili nchini Ethiopia, akiwa rais wa kwanza wa Marekani kuitembelea nchi hiyo akiwa madarakani. Wanaharakati wanahofia ziara hiyo itaipa uhalali serikali yao inayoongoza kiimla.

https://p.dw.com/p/1G4wT
Rais Barack Obama wa Marekani ambaye yuko ziarani katika mataifa ya kiafrika.
Rais Barack Obama wa Marekani ambaye yuko ziarani katika mataifa ya kiafrika.Picha: Getty Images/AFP/S. Loeb

Kama ilivyokuwa kwa Kenya, ziara ya rais Barack Obama nchini Ethiopia itakuwa ya kwanza kufanywa na rais wa Marekani aliyeko madarakani, na kwa kulingana na maoni ya serikali mjini Addis Ababa, hiyo ni ishara ya kupanda kwa hadhi ya nchi hiyo.

Wanasiasa wa upinzani nchini Ethiopia wameelezea wasiwasi kwamba ziara ya Obama katika nchi hiyo yenye wakazi milioni 90, ambayo inakuja siku chache tu baada ya chama tawala nchini humo kupata ushindi wa asilimia 100 katika uchaguzi wa bunge, itaipa uhalali serikali ya nchi hiyo ambayo inaongozwa na sera za ukandamizaji.

Kutokana na siasa za uzalendo wa kiafrika, Ethiopia ni mwenyeji wa makao makuu ya Umoja wa Afrika, ambapo rais Obama atatoa hotuba kwa bara zima la Afrika Jumanne ijayo.

Uimara wa Ethiopia watambuliwa?

Waziri wa habari wa Ethiopia Redwan Hussein amesema ingawa hii ni mara ya kwanza kwa rais wa Marekani aliyeko madarakani kuitembelea nchini hiyo, Marekani na Ethiopia zimekuwa na uhusiano wa kibiashara tangu mwaka 1903. Waziri huyo ameongeza kwamba uamuzi wa rais wa Marekani kuitembelea Ethiopia unatokana na kwamba umuhimu wa Ethiopia umeongezeka na Marekani inalitambua hilo.

Serikali ya Ethiopia inakosolewa kuukandamiza upinzani
Serikali ya Ethiopia inakosolewa kuukandamiza upinzaniPicha: picture-alliance/dpa/M. Wondimu Hailu

Lakini, ingawa waziri huyo anasema wizara ya rais Obama itatoa hamasa kwa raia wa Ethiopia, mtafiti katika Taasisi ya taaluma ya usalama Hallellujah Lulie anasema ziara hiyo haitabadilisha chochote.

''Unachotakiwa kufanya tu ni kuziangalia ripoti mbali mbali za wizara ya mambo ya nje ya Marekani, ambazo zinamulika visa vya ukiukaji wa haki za binadamu, kuwaweka watu kizuizini kinyume cha sheria, utesaji, hata mauaji dhidi ya wapinzani, waandishi wa habari na mabloga. Siamini kwamba wizara ya Obama itatoa mchango wowote mkubwa katika kuyashughulikia matatizo hayo''. Amesema Lulie.

Mazungumzo ya kuambiana ukweli

Nchini Ethiopia rais Obama atafanya mazungumzo na rais wa nchi hiyo Mulatu Teshome na waziri mkuu Hailemariam Desalegn. Mazungumzo hayo yatauangazia mzozo wa Sudan Kusini, mapambano dhidi ya kundi la al-Shabab nchini Somalia, pamoja na miradi ya maendeleo.

Maafisa pia wameahidi kuwepo kwa hali ya kuambiana ukweli juu ya ukandamizaji wa vyombo vya habari, na mbinyo dhidi ya upinzani wa kisiasa.

Mwezi Mei mwaka huu chama kilichoko madarakani kilipata ushindi wa asilimia 100 katika uchaguzi wa bunge ambao ulitajwa na Marekani pamoja na Umoja wa Ulaya kutokuwa wa haki.

Kiongozi wa chama cha upinzani kijulikanacho kama Blue Party Woretaw Wassie, amesema maafisa wa chama chache wamekamatwa kabla ya ziara ya rais Obama, huku serikali ikihofu kwamba wangeweza kusabisha fujo.

Suala jingine lenye utata katika mazungumzo baina ya rais Obama na wenyeji wake nchini Ethiopia litakuwa juu ya haki za watu wanaofanya mapenzi ya jinsia moja, ambalo Obama aliligusia wakati wa ziara yake nchini Kenya jana, akitoa wito wa kuwepo kwa sheria inayowapa watu wote haki sawa.

Wapinzani wa haki za mashoga wametaka dini zote nchini Ethiopia ziungane dhidi ya rais Obama, ikiwa ataanza kuyataja masuala ya ushoga.

Mwandishi: Daniel Gakuba/ape/rtre

Mhariri: Mohamed Dahman