1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama azindua mkakati mpya wa kijeshi

Caro Robi6 Januari 2012

Rais wa Marekani Barrack Obama amezindua mkakati wa ulinzi ambao utapanua uwezo wa jeshi la Marekani barani Asia, lakini utapunguza idadi jumla ya wanajeshi wake katika jeshi hilo ili liwe na ufanisi zaidi.

https://p.dw.com/p/13fCg
Rais Barack Obama wa Marekani akitangaza mkakati mpya wa kijeshi wa nchi yake kwenye makao makuu ya jeshi, Pentagon.
Rais Barack Obama wa Marekani akitangaza mkakati mpya wa kijeshi wa nchi yake kwenye makao makuu ya jeshi, Pentagon.Picha: dapd

Mkakati huo endapo utatekelezwa, utalibadilisha kwa kiasi kikubwa jeshi hilo la Marekani linaloaminika kuwa lenye nguvu zaidi duniani, kufuatiwa kuimarishwa wakati wa utawala wa rais George W. Bush alipoanzisha kampeni ya vita dhidi ya ugaidi nchini Iraq na Afghanistan.

Matumizi ya teknolojia ya mitandao kupigana vita na ndege zisizoendeshwa na marubani zitaendelea kupewa kipaumbele, huku makabiliano dhidi ya China na Iran ambao wanajaribu kupinga mipango ya Marekani katika maeneo kama kusini mwa bahari ya China na mlango wa bahari wa Hormuz.

Lakini kikosi cha Marekani, silaha za kinyuklia na kuwepo katika mataifa ya barani Ulaya vitapungua, hasa nchini Ujerumani, ambapo wana wanajeshi 43,000. Marekani inanuia kupunguza matumizi ya fedha kwa karibu dola bilioni 487 katika kipindi cha muongo mmoja ujao.

Hivi karibuni, kikosi cha Jeshi la Marekani kilijiondoa kutoka Afghanistan baada ya kuwepo katika nchi hiyo kwa miaka kumi.

Jeshi hilo tayari linapanga kupunguza idadi ya wanajeshi wanaohudumu katika mataifa ya kigeni kutoka 565,000 hadi 520,000 kufikia mwaka 2014. Wachambuzi wengi wanasema idadi hiyo itapungua hata zaidi.

Vikosi vya Marekani vikijitayarisha kuondoka nchini Iraq katikati ya mwezi Disemba 2011.
Vikosi vya Marekani vikijitayarisha kuondoka nchini Iraq katikati ya mwezi Disemba 2011.Picha: dapd

Mkakati huo utapelekea idadi ya wanajeshi kurejea katika hali iliyokuwa kabla ya mashambulizi ya kigaidi ya tarehe 11 mwezi septemba mwaka 2001.

Kabla ya hapo, jeshi la nchi kavu lilikuwa na kikosi cha wanajeshi 482,000 na jeshi la majini lilikuwa na wanajeshi 173,000.

Kwa jumla, jeshi la Marekani lina wanajeshi milioni 1.4, ikilinganishwa na jeshi la China ambalo lina wanajeshi milioni 2.3 na Korea Kaskazini lililo na wanajeshi milioni 1.1.

Huku Marekani ikifuatilia kwa makini kukua kwa haraka kwa China kijeshi na kiuchumi, jeshi la nchi yake lina mipango ya kujizatiti hasa katika eneo la Asia na Bahari ya Pacifik ili kuhakikisha maslahi yake, hasa ya kibiashara, hayatatizwi ikiwemo katika bahari ya China Kusini.

Rais Barack Obama akihutubia wanajeshi wa Marekani katika Ngome ya Bragg siku moja kabla ya wanajeshi wa Marekani kuondoka rasmi nchini Iraq, 14 Disemba 2011.
Rais Barack Obama akihutubia wanajeshi wa Marekani katika Ngome ya Bragg siku moja kabla ya wanajeshi wa Marekani kuondoka rasmi nchini Iraq, 14 Disemba 2011.Picha: dapd

Kufuatia hayo, matumizi ya wizara ya ulinzi ya Marekani yataelekeza fedha zake kwa ndege zisizotumia rubani, matumizi ya silaha za kielektroniki na silaha za kutumika katika vita vya majini, na pia kuboresha uhusiano wa kiulinzi na washirika wao wa karibu katika eneo hilo la Asia na Pacifik, kama Indonesia.

Rais Obama jana, akizundua mkakati huo, alisema kuwa hautaathiri bajeti ya ulinzi na kwamba matumizi yake yatakuwa kushinda hata wakati wa utawala wa Bush, licha ya kuwa watapunguza idadi ya wanajeshi.

Anataka ulimwengu ujue kuwa bado jeshi la nchi yake litakuwa na nguvu zaidi ya lolote lile. Matumizi ya jeshi lake katika kipindi cha mwaka huu cha matumizi ya fedha za serikali ni karibu dola bilioni 530, ukiachilia mbali matumizi ya jeshi lake nchini Afghanistan, ikiwa ni karibu asilimia 40 ya matumizi ya kijeshi kote ulimwenguni.

Mwandishi: Caro Robi/Reuters/AFP
Mhariri: Othman Miraji