1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama katika ziara ya kihistoria Cuba

Iddi21 Machi 2016

Rais wa Marekani Barack Obama yuko nchini Cuba kwa ziara ya kihistoria, akifungua ukurasa mpya katika ushirikiano wa mataifa hayo, baada ya miongo kadhaa ya uhasama baina ya maadui hao wa zamani wa vita baridi.

https://p.dw.com/p/1IGkK
Rais Barack Obama na familia yake baada ya kuwasili mjini Havana siku ya Jumapili.
Rais Barack Obama na familia yake baada ya kuwasili mjini Havana siku ya Jumapili.Picha: Y. Cortez/AFP/Getty Images

Ziara hiyo ya siku tatu, na ya kwanza kufanywa na Rais wa Marekani nchini Cuba katika kipindi cha miaka 88, ni matokeo ya ufunguaji wa kidiplomasia uliyotangazwa na Obama na Rais wa cuba Raul Castro Desemba 2014, na kuhitimisha enzi ya vita baridi iliyoanza baada ya mapinduzi ya Cuba kuiangusha serikali rafiki na Marekani mwaka 1959.

Obama ambaye aliachana na sera ya muda mrefu ya Marekani ya kujaribu kuitenga Cuba, anataka kuyafanya mabadiliko hayo yawe ya kudumu. Lakini bado kuna vikwazo kadhaa katika njia ya kurejesha uhusiano kamili, na wakosoaji wa Rais huyo Mdemokrat wanasema ziara hiyo imefanywa kwa pupa. Obama ameambatana na mke wake Michelle, mama mkwe wake pamoja na binti zao Sasha na Malia.

Kina Obama wakisalimia na wafanyakazi wa ubalozi wa Marekani mjini Havana.
Kina Obama wakisalimia na wafanyakazi wa ubalozi wa Marekani mjini Havana.Picha: N. Kamm/AFP/Getty Images

"Kwa mara ya kwanza kabisa AirForce One imetua nchini Cuba na hiki ndicho kituo chetu cha kwanza, hivyo hii ni ziara ya kihistoria na ni fusra ya kihistoria kushiriki moja kwa moja na watu wa Cuba na kujenga mahusiano mapya na makubaliano ya kibishara, na kuimarisha uhusiano kati ya watu wetu. Na kwangu ni kuainisha dira yangu ya mustakabali mwema kuliko yaliyopita," alisema Obama wakati akizungumza na wafanyakazi wa ubalozi wa Marekani mjini Havana.

Hakuna mkutano na Fidel Castro

Obama atakuwa na mazungumzo na Rais Raul Castro - lakini siyo na kaka yake Fidel, kiongozi wa mapinduzi ya mwaka 1959. Atazungumza pia na wajasiriamali, kukutana kwa faragha na wapinzani, kuwahutubia Wacuba moja kwa moja kupitia vyombo vya habari vya serikali na pia atahudhuria mechi ya maonyesho ya besiboli siku ya Jumanne.

Ziara hii ni ya kiishara lakini pia ina maana kubwa baada ya miongo kadhaa ya uhasama kati ya Washington na Havana. Inamfanya Obama kuwa Rais wa kwanza wa Marekani alieko madarakani kuizuri Cuba tangu Calvin Coolidge alipowasili nchini humo kwenye meli ya kivita mwaka 1928.

Vile vile ni fursa nyingine ya kuondoa vikwazo vilivyosalia juu ya biashara ya Cuba na usafiri, na kujenga uhusiano wa kawaida kati ya Washington na Havana. Tangu zilipoanza kukaribiana, nchi hizo mbili zimerejsha uhusiano wa kidiplomasia na kusaini makubaliano ya kibishara katika nyanja za mawasiliano na huduma za safari za ndege.

Obama na familia wakiuzuru mji wa kale wa Havana kwa miguu licha ya mvua.
Obama na familia wakiuzuru mji wa kale wa Havana kwa miguu licha ya mvua.Picha: Reuters/C. Barria

Kerry kukutana na Wacolombia

Tofauti kubwa bado zinaendelea kuwepo, moja wapo ikiwa vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Cuba vilivyodumu kwa miaka 54. Obama ameliomba bunge la Marekani- Congress liondowe vikwazo hivyo, lakini hatua hiyo imetiliwa guu na uongozi wa chama cha Republican.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry, ambaye pia yumo katika msafara wa Rais Obama, atatumia fursa hiyo kukutana mjini Havana na wapatanishi wa serikali ya Colombia pamoja na waasi FARC wanaojaribu kufikia muafaka utakaokomesha vita vya nusu karne nchini Colombia.

Kerry amesema anataka kuona maendeleo yaliyofikiwa katika majadiliano baina ya pande hizo mbili. Wajumbe wa majadiliano hayo yanayofanyika katika mji mkuu wa Cuba tangu Novemba 2012 -- wametangaza hatua kadhaa walizofikia katika miezi ya karibuni, lakini makubaliano ya mwisho bado kufikiwa.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe,ape,rtrtv

Mhariri: Caro Robi