1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama na Clinton watoa wito kuleta mageuzi Marekani

C.Bergmann - (P.Martin)30 Oktoba 2008

Marekani,siku sita kabla ya uchaguzi wa Novemba 4,bingwa wa zamani wa Demokratik Bill Clinton na bingwa mpya Barack Obama waliweka kando tofauti zao na wakasimama pamoja kutoa wito uliosisimua kuleta mageuzi nchini humo.

https://p.dw.com/p/FkM9
In this image from video provided by the Obama Campaign, Democratic presidential candidate Sen. Barack Obama., speaks during a 30-minute infomercial to be broadcast on prime-time television Wednesday, Oct. 29, 2008. (AP Photo/Obama Campaign)
Mgombea urais wa chama cha Demokratik,Barack Obama katika tangazo la dakika 30 kwenye televisheni,akifanya kampeni ya uchaguzi wa Marekani.Picha: AP

Kwenye mkutano wao wa kwanza wa pamoja uliofanywa Jumatano usiku kwenye bustani mjini Orlando,rais wa zamani Clinton alisema,Obama ni mustakabali wa Marekani na akauhimiza umati wa kama watu 35,000 kumshinda John McCain wa chama cha Republikan katika uchaguzi utakaofanywa Jumanne ijayo.

Clinton ambae mkewe Hillary Clinton alishindwa na Obama katika kinyanganyiro cha awali kugombea urais kwa tikti ya chama cha demokratik,aliweka kando kinyongo chake alipomuidhinisha Obama kwenye mkutano mkuu wa chama hicho hapo mwezi Agosti.Na hiyo jana alipohotubia mkutano wa Orlando,aliuambia umati uliokusanyika,iwapo uamuzi wao utapitishwa kwa kuzingatia nani atakaewatoa kutoka janga la hivi sasa,basi ni dhahiri kuwa Barack Obama ndio awe rais ajae na hilo lawezekana kwa msaada wao.Vile vile akashambulia jinsi uchumi ulivyoporomoka chini ya uongozi wa chama cha Republikan na akaulinganisha mgogoro wa fedha unaokabiliwa na Marekani hivi sasa na uchumi uliyostawi wakati wa uongozi wake katika miaka ya tisini.Akaeleza kuwa Obama,ameukabili mgogoro huo wa fedha kwa kuwaendea washauri wake na hata maafisa wa enzi ya Clinton kushauriwa njia bora ya kulisaidia taifa badala ya kujinufaisha kisiasa.Na hivyo ndio rais anavyopaswa kutenda anapokabiliwa na mgogoro - kuchukua hatua itakyoinufaisha Marekani.

Kwa upande wake Barack Obama,alietumia hadi dola milioni tatu kwa matangazo ya nusu saa kwenye stesheni saba za televisheni kote Marekani kufanya kampeni ya uchaguzi alisema,wakati umewadia kuwa na amani na ustawi wa kiuchumi kama ilivyoshuhudiwa katika miaka ya tisini na kuongezea:

"Fedha zinazotumiwa huko Irak hii leo ni zaidi kuliko hapo mwanzoni mwa vita hivyo.Shule ngapi zingeweza kujengwa kwa pesa hizo; hospitali ngapi; watu wangapi wangeweza kupatiwa huduma za afya; vijana wangapi wangeweza kusaidiwa kuendelea na masomo.Sasa wakati umewadia kutumia sehemu ya fedha hizo nchini Marekani."

Kwa mujibu wa tarakimu zilizotolewa na CNN kuhusu uchunguzi wa maoni uliofanywa,Obama yupo mbele ya mpinzani wake John McCain wa Republikan.Lakini bado hajashinda uchaguzi kwa hivyo kampeni za kuwavutia wapiga kura zinaendelea.