1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama na Merkel wazungumzia sakata ya udokozi wa Marekani

Admin.WagnerD4 Julai 2013

Rais wa Marekani Barack Obama, ametafuta kuondosha wasiwasi wa Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, kuhusu madai ya mpango wa udokozi wa Marekani dhidi ya washirika wake wa Ulaya

https://p.dw.com/p/191zf
Picha: Reuters

Umoja wa Ulaya umeitaka Marekani kujieleza kutokana na ripoti iliyochapishwa katika gazeti moja la Ujerumani kuwa Marekani inawachunguza washirika wake barani Ulaya na kuuita mpango huo wa kushutusha kama ni kweli.

Ripoti hiyo ilitokana na ufichuzi wa mfanyikazi wa zamani wa kijasusi Edward Snowden ambaye amekwama katika uwanja wa ndege wa Moscow akitafuta kusafiri hadi kwa nchi itakayompa hifadhi huku Marekani ikiishinikiza Urusi kumrejesha nyumbani.

Taarifa kutoka ikulu ya Rais Obama imesema Merkel na Obama wamefanya mazungumzo kwa njia ya simu wiki mbili tu baada ya kukutana ana kwa ana mjini Berlin.

Taarifa hiyo inasema Rais Obama anachukulia kwa uzingativu mkubwa wasiwasi wa washirika wake wa Ulaya na kwamba maafisa wa Marekani na umoja wa Ulaya watajadili masuala ya kijasusi na mengine ya faragha pengine hata kabla ya tarehe 8 mwezi huu.

Mfichua siri za Marekani Edward Snowden
Mfichua siri za Marekani Edward SnowdenPicha: The Guardian/Getty Images

Msemaji wa Kansela Merkel, Steffen Seibert, amesema mazungumzo huru kati ya Marekani na Umoja wa Ulaya yanasalia kupewa kipaumbele baada ya mazungumzo kupitia simu kati ya Merkel na Rais Obama na kuongeza viongozi hao wawili wote wamethibitisha nia yao kuu ya kuweko kwa mkutano uliopangwa wa ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji kati ya Marekani na Ulaya ambao utaanza Jumatatu ijayo.

Ujerumani na Marekani kuendeleza ushirikiano

Seibert amesema ziara inayotarajiwa mjini Washington ya ujumbe wa wawakilishi kutoka wizara mbali mbali za Ujerumani itatoa fursa ya mazungumzo ya kina kuhusiana na masuala hayo pamoja na mazungumzo ya kuendeleza ushirikiano hata zaidi.

Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani, Hans-Peter Friedrich, amesema wawakilishi hao ambao ni wa kiwango kinachofuata manaibu mawaziri watathimini vyanzo vya mawasiliano yanaoingia Ujerumani ili kuwalinda raia wake.

Msemaji wa Kansela wa Ujerumani Steffen Seibert
Msemaji wa Kansela wa Ujerumani Steffen SeibertPicha: picture alliance/dpa

Hata hivyo kiongozi wa chama cha upinzani cha Social Democtaic, SPD, katika bunge la Ujerumani, Thomas Oppermann, ameshutumu chaguo la Merkel la wajumbe hao na kusema Kansela huyo anahitaji kufanya mashauriano muafaka ya kiserikali kwani ni suala la kisiasa.

Ghadhabu kutokana na ufichuzi wa hivi punde kuwa Marekani imekuwa ikizichunguza nchi za Umoja wa Ulaya unatishia kusambaratisha mkutano ambao ndio mkubwa zaidi wa makubaliano ya kibiashara kati ya Marekani na Umoja wa Ulaya kuwahi kuafikiwa.

Ufaransa imetaka mkutano huo kuahirishwa kwa muda kutokana na madai ya mfichua siri Edward Snowden, ambaye sasa anatafutwa, lakini Rais wa halmashauri ya umoja wa Ulaya, Jose Manuel Barrosso, amesema mazungumzo hayo yataendelea kama yalivyopangwa sambamba na makundi yaliyotwikwa jukumu la kufanya uchunguzi kubaini athari ya udokozi huo wa Marekani.

Mwandishi: Caro Robi/afp/reuters

Mhariri: Josephat Charo