1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama na washirika wa ghuba waahidi kuiangamiza IS

Admin.WagnerD21 Aprili 2016

Marekani na washirika wake wa mataifa ya ghuba wameahidi kuendelea kufanyakazi kwa pamoja kupambana na kundi la Dola la Kiislamu na kupunguza mizozo mingine ya eneo hilo, amesema Rais Barack Obama leo(21.04.2016).

https://p.dw.com/p/1IaPS
Saudi-Arabien Riad Besuch Barack Obama
Obama akizungumza baada ya kushiriki kikao cha baraza la ushirikiano la mataifa ya ghubaPicha: Reuters/K. Lamarque

Hata hivyo amesisitiza kwamba wasi wasi unaendelea kuwapo kuhusiana na Iran na masuala ya kiuchumi ikiwa ni pamoja na mafuta.

Katika kile ambacho huenda ni ziara yake ya mwisho akiwa rais kwa washirika wa kihistoria wa Marekani, Obama ametaka kuondoa hali ya wasi wasi na mataifa hayo ya Kisunni , wasi wasi uliojikita katika mtazamo wa marekani kuelekea hasimu wao mkubwa katika eneo hilo, Iran ya Kishia.

Saudi-Arabien Barack Obama Gipfelkonferenz des Golf-Kooperationsrates in Riad
Barack Obama akiwa na Mfalme Salman wa SaudiaPicha: Reuters/F. Al Nasser

IS yaendelea kupoteza maeneo

Wakati kundi la Dola la Kiislamu likiathirika kwa kupoteza maeneo katika maeneo mbali mbali yaliyo chini ya udhibiti wake nchini Syria na Iraq, Marekani inatafuta msaada zaidi kutoka mataifa tajiri ya kifalme katika eneo la ghuba ili kuendeleza mbinyo dhidi ya kundi hilo.

"Tunaendelea kuwa pamoja katika vita vya kuliangamiza kundi la IS ama Daesch, ambalo ni kitisho kwetu sote. Na Marekani itawasaidia washirika wetu wa GCC kuhakikisha vikosi vyao maalum vinapata vifaa. Na mataifa ya GCC yanaendelea kutoa mchango wao katika mapambano dhidi ya IS na muungano tuliouanzisha."

Saudi Arabia na mataifa mengine ya ghuba yamo katika muungano unaoongozwa na Marekani unaofanya mashambulizi ya anga dhidi ya kundi la IS nchini Syria na Iraq tangu katikati ya mwaka 2014.

Saudi-Arabien Barack Obama Gipfelkonferenz des Golf-Kooperationsrates in Riad
Obama akizungumza na waziri mkuu wa Oman Sayyid Fahd bin Mahmaoud al SaidPicha: Reuters/K. Lamarque

Matumaini katika mazungumzo

Syria, ambako Saudi Arabia na washirika wake wa Kisunni wamekuwa wakiunga mkono upinzani , ni suala ambalo pia limejadiliwa katika mkutano huo wa kilele.

Marekani ina matumaini kwamba usitishaji mapigano , na mazungumzo ya amani mjini Geneva , vinaweza kusaidia kutatua mzozo mkubwa wa Syria na kuelekeza mtazamo wake katika mapambano dhidi ya kundi la IS na makundi mengine ya jihadi. Matumaini hayo pia yako nchini Yemen.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry pia alijiunga na Obama mjini Riyadh, ambako alikuwa na mazungumzo na naibu mwana mfalme mteule na waziri wa ulinzi Mohammed bin Salman.

Saudi-Arabien Barack Obama Gipfelkonferenz des Golf-Kooperationsrates in Riad
Kikao cha baraza la ushirikiano la mataifa ya ghuba kikiendeleaPicha: Reuters/K. Lamarque

Marekani na kundi la mataifa ya GCC itaanzisha majadiliano mapya ya kiwango cha ngazi za juu ya kiuchumi yakiwa na mtazamo kuhusiana na kuweka sawa bei za chini za mafuta, kuongeza mahusiano ya kiuchumi na kuunga mkono mageuzi ya mataifa ya baraza la ushirikiano la mataifa ya ghuba wakati wakifanyakazi kujenga nafasi za ajira na fursa kwa vijana na raia wote kwa jumla, Obama amesema katika matamshi kufuatia mkutano huo wa kilele wa GCC.

Obama anaondoka leo mjini Riyadh ambapo anatarajiwa kuelekea nchini Uingereza kwa ziara ya siku mbili.

Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre , afpe

Mhariri:Gakuba Daniel