1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama ziarani Mashariki ya Kati.

Nyanza, Halima21 Julai 2008

Mgombea Urais nchini Marekani kupitia chama cha Democratic, Barack Obama amewasili nchini Iraq, baada ya kutembelea Kabul na Kuwait ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kutembelea mashariki ya kati.

https://p.dw.com/p/Eg77
Mgombea wa Urais nchini Marekani kwa tiketi ya chama cha Democratic, Barack Obama, ziarani Mashariki ya Kati, ambapo pia atatembelea nchi za Ulaya ikiwemo Ujerumani.Picha: AP/DW

Ziara hiyo ya Barack Obama nchini Iraq, ni ya pili katika eneo linalokabiliwa na mapigano, ambapo alianza na Afghanistan.

Ziara hiyo pia ya Mgombea huyo wa kiti cha Urais nchini Marekani, ambayo ni sehemu ziara ya wajumbe wa baraza la Congress imegubikwa na usiri kutokana na sababu za kiusalama, lakini atakutana na makamanda wa ngazi za juu wa jeshi la Marekani, wanadiplomasia pamoja na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Nouri Al Maliki.

Barack Obama anaitembelea Iraq katika kipindi ambacho mipango yake ya kuondoa majeshi ya Marekani nchini humo ndani ya kipindi cha miezi 16 atakaposhika madaraka, imezua utata.

Waziri Mkuu wa nchi hiyo Nouri Al Malik ametengua maelezo yake ya awali ambayo yalichapishwa katika gazeti moja la Ujerumani mwishoni mwa wiki, ambapo alinukuliwa akisema anaungana na Barack Obama katika mpango wa kuwaondoa wanajeshi hao nchini mwake.

Msemaji wa serikali ya Iraq, Ali Dabagh alikanusha kwa kusema kuwa maelezo ya Waziri Mkuu huyo hayakueleweka na kwamba yalitafsiriwa vibaya.

Maelezo hayo yaliyoripotiwa ya Bwana Malik yamekuja suku moja tu, baada ya Rais George W Bush wa Marekani kukubali kile kilichoitwa ratiba pana ya kuondoa majeshi yake kutoka Iraq, ambayo haina muda maalum.

Kwa upande mwingine Wairaq wamegawanyika juu ya mpango huo wa Barack Obama, kutokana na baadhi yao kuona kama sehemu ya kampeni za uchaguzi ili kupata kura za Wamarekani waliochoshwa na vita na kwamba wengine wanahofia athari zitakazoweza tokea baada ya kuondolewa haraka kwa majeshi hayo nchini humo.

Akiwa nchini Afghanistan, Barack Obama alisema hali ilivyo nchini humo ni mbaya na inahitaji utatuzi wa dharura.

Aliongeza kusema kuwa Marekani inapaswa kuanza mpango wa kuwahamishia huko wanajeshi zaidi kutoka Iraq.

Afghanistan imekuwa ikipambana na vikundi vya wapiganaji wa Kitaliban pamoja na kundi la Al Qaida nchini humo, ambapo Marekani imekuwa ikisaidia serikali ya nchi hiyo kupambana na wapiganaji hao.

Ziara hiyo ya Barack Obama katika nchi za kigeni inalenga kumuongezea utambulisho katika sera za kigeni, ambapo pia wiki hii atatembelea nchi nyingine za mashariki ya kati ikiwemo Isreal, na baadhi ya mataifa yenye nguvu barani Ulaya, ambapo alhamisi anatarajiwa kutembelea Ujerumani na kwamba anatarajiwa kuhutubia mjini Berlin.