1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama ziarani Mashariki ya kati

Oumilkher Hamidou4 Juni 2009

Rais Barack Obama azungumza na rais Mubarack wa Misri

https://p.dw.com/p/I3KR
Rais Obama anaamkiana na rais MUbarackPicha: AP

Rais Barack Obama wa Marekani amewasili Cairo leo anakotazamiwa kutoa hutuba inayosubiriwa sana ya suluhu na ukurasa mpya wa uhusiano kati ya Marekani na ulimwengu wa kiislam.

Akitokea Saud Arabia,mshirika mwengine wa Marekani na shina la dini ya kiislam,rais Barack Obama amewasili Cairo saa tatu za asubuhi hii leo kwa ziara muhimu ya saa sabaa.

Hakuna hata kiumbe mtu anachokiona njiani katika mji mkuu huo wa Misri,wenye wakaazi milioni 20,-kwakua siku ya leo imetangazwa kua ni siku ya mapumziko.Vikosi vya polisi vinapiga doria katika kila pembe.Amepokelewa uwanja wa ndege na waziri wa mambo ya nchi za nje Ahmed Abou Gheith kabla ya kwenda katika kasri la Qobba kwa mazungumzo pamoja na rais Hosni Mubarak .

Rais Obama amewaambia waandishi habari baada ya mazungumzo yake,mara baada ya kuwasili "amezungumza ana kwa ana pamoja na rais Mubarak " mwenye miongo kadhaa ya maarifa" kuhusu njia za kufufua utaratibu wa amani kati ya Israel na waarabu.

"Marekani imedhamiria kushirikiana na nchi zote za eneo hili ili kukidhi matarajio ya wote" amesisitiza rais Obama,aliyefafanua wamezungumzia pia "hali kati ya waisrael na Palastina.

Obama in Ägypten
Rais Mubarak anamkaribisha rais Obama katika kasri la QoobaPicha: AP

Kwa upande wake rais Hosni Mubarak amesema wamejadiliana "kwa dhati na bila ya kificho kuhusu masuala yanayohusu Mashariki ya kati,ikiwa ni pamoja na Iran inayotuhumiwa na nchi za magharibi kutaka kutengeneza silaha za kinuklea.

Baadae rais Obama alitembelea msikiti Sultan Hassan,jengo la enzi za kati,kabla ya kwenda katika chuo kikuu mashuhuri cha mjini Cairo ambako wawakilishi zaidi ya elfu tatu wanamsubiri.

Huko ndiko rais Barack Obama anakotarajiwa kutoa hotuba inayosubiriwa kwa hamu na waislam zaidi ya bilioni moja na nusu kote ulimwenguni.

Ingawa hotuba hiyo haitazamiwi kufafanua mkakati madhubuti wa kuufumbua mzozo kati ya Israel na Palastina,hata hivyo wengi wanaamini hotuba hiyo itatoa mwito wa suluhu.

Macho ya wanamtandao yamelengwa katika tovuti ya Facebook,Twitter na Myspace huku mtandao wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani ukijiandaa kutuma sehemu za hotuba hiyo kupitia SMS kwa lugha ya kiarabu,kifarsi,Urdu na kiengereza.

Baada ya hotuba hiyo rais Obama atatembelea bonde la Guizeh kujionea piramidi tatu kubwa.

Haijulikani bado kama rais Obama atakua na mazungumzo pia na wanaharakati wa mashirika ya jamii au na upande wa upinzani.

Nchini Israel ziara hii ya rais Obama inaangalwa kijicho upembe,kuna wanaohofia Marekani isije ikaelemea zaidi upande wa ulimwengi wa kiarabu .

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir / AFP

Mhariri:Abdul Rahman