1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ocampo ataka kuchunguzwa kwa wahusika wa ghasia za Kenya

Mohamed Dahman26 Novemba 2009

Mwendesha mashtaka mkuu wa mahkama ya kimataifa ya uhalifu wa Kivita Luis Moreno- Ocampo aomba majaji kuruhusu uchunguzi juu ya uhalifu dhidi ya ubinaadamu uliotendeka Kenya mwaka 2008.

https://p.dw.com/p/KhEl
Luis Moreno Ocampo, mwendesha mashtaka mkuu wa mahkama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita ICC.Picha: AP

Mwendesha mashtaka mkuu wa Mahkama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita amesema hapo Alhamisi kwamba atawaomba majaji kuruhusu uchunguzi rasmi wa ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 nchini Kenya kwa nia ya kuwafikisha mahkamani wahusika wa ghasia hizo.

Ocampo amewaambia waandishi wa habari mjini The Hague Uholanzi kwamba kulikuweko na mashambulio ya makusudi dhidi ya raia yaliozagaa nchini kote Kenya ambayo ni uhalifu dhidi ya ubinaadamu kama vile ubakaji, mauaji,kuhamisha watu kwa nguvu na kuwapotezea makaazi wengine.

Mwendesha mashtaka huyo mkuu wa Mahkama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita alikuwa akifanya uchunguzi wa awali tokea mwezi wa Februari mwaka jana juu ya ghasia hizo zilizozuka kufuatia uchaguzi wa rais uliofanyika tarehe 27 mwezi wa Desemba mwaka 2007 baada ya kiongozi wa upinzani Raila Odinga kumtuhumu Rais Mwai Kibaki kwa kuhujumu uchaguzi huo.Takriban wtu 1,500 waliuwawa na 300,000 walipotezewa makaazi yao katika kipindi cha wiki chache.

Ocampo alikua anakusudia kuwasilisha kesi chache katika mahkama hiyo dhidi ya wale wanaobeba jukumu kuu la ghasia hizo ,wale walioandaa,waliopanga na kuunga mkono mashambulio hayo dhidi ya raia.

Hii ni mara ya kwanza kwamba mwendesha mashtaka wa mahkama hiyo anataka kuanzishwa kwa uchunguzi kwa juhudi zake mwenyewe binafsi mojawapo ya njia tatu ambapo kwayo kesi inaweza kuwasilishwa mbele ya Mahkama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita ICC. Anahitaji ruhusa ya majaji kuweza kufanya hivyo.

Kesi nyengine zilioko katika mahkama hiyo aidha zimewasilishwa na nchi ambazo zimesaini Sheria ya Rome ilioanzisha mahkama hiyo au na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kama vile ilivyo kesi ya mzozo wa Dafur nchini Sudan. ICC tayari imewateuwa majaji watatu kufikiria ombi hilo la mwendesha mashtaka kuhusiana na kesi ya Kenya.

Serikali ya Kenya bado haikuchukua hatua juu ya pendekezo lake yenyewe la uchunguzi wa mwaka mzima kwamba kuanzishwe mahkama maalum kuchunguza ghasia hizo. Mapema mwezi huu Waziri wa mambo ya nje wa Kenya Moses Wetangula amesema kwamba serikali ya Kenya itaisaidia mahkama hiyo ya ICC kufanya uchunguzi lakini imeazimia kutafuta ufumbuzi wa ndani ya nchi juu ya suala hilo.

Mahkama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita,mahkama pekee huru duniani kuendesha kesi za uhalifu wa vita,uhalifu dhidi ya ubinaadamu na mauaji ya kimbari ilianza kazi hapo mwaka 2002 mjini The Hague. Mahkama hiyo inaweza tu kuendesha kesi pale nchi zinapokuwa haziko tayari au kushindwa kufanya hivyo.

Moreno Ocampo tayari alikuwa ametangaza hapo mwezi wa Septemba nia yake ya kuwashughulikia wale waliohusika na ghasia za Kenya.

Hapo mwezi wa Juni Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan ameitaka Kenya kuunda mahkama maalum kujaribu kuwafungulia mashtaka watu hao venginevyo iwafikishe katika mahkama ya ICC.

Annan msuluhishi mkuu katika mazungumzo ya kugawana madaraka nchini Kenya ambayo yamemuwezesha Odinga kuwa waziri mkuu na Kibaki kuendelea kuwa rais aliipelekea mahkama hiyo orodha ya majina ya watuhumiwa wakuu hapo mwezi wa Julai ambayo inaaminika kuwa kuwajumuisha viongozi wa juu wa serikali ya Kenya.


Mwandishi:Mohamed Dahman /AFP

Mhariri: Aboubakary Liongo